Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ziarani Sweden, Finland
13 Februari 2023Ziara hiyo imetawaliwa na mkwamo wa maombi ya nchi hizo kutaka kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO na vilevile mjadala kuhusu msaada wa silaha kwa Ukraine. Serikali ya Ujerumani inatafuta kundi la washirika ambao wako tayari kuipa Ukraine vifaru vya kivita.
Katika mji mkuu wa Finland Helsinki, Baerbock atafanya mkutano na waziri wa nje wa nchi hiyo Pekka Haavisto, na pia atazuru kituo cha kiraia cha ulinzi kilichoko chini ya ardhi.
Kesho Jumanne, Baerbock ataendelea na ziara yake hadi Stockholm, mji mkuu wa Sweden.
Sweden na Finland ziliwasilisha maombi ya kujiunga na NATO karibu mwaka mmoja uliopita.
Lakini ni shuruti nchi zote 30 ambazo ni wanachama wa jumuiya hiyo ziridhie maombi hayo. Kwa sasa Uturuki na Hungary hazijaidhinisha maombi hayo.