1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine kuzuru China

22 Julai 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba kuanzia tarehe 23 hadi 25 Julai ataitembelea China kutokana na mwaliko aliopewa na nchi hiyo.

Ukraine Dmytro Kuleba
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro KulebaPicha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, atafanya mazungumzo na mwenzake wa China Wang Yi katika ziara yake hiyo itakayoanza hapo tarehe 23 hadi tarehe 25 Julai.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine mazungumzo hayo yatazingatia jinsi ya kuvimaliza vita vya Urusi nchini Ukraine na juu ya uwezekano wa jukumu la China katika kufikia makubaliano ya kuvimaliza vita hivyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning, amesema mwaliko huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang YiPicha: Willy Kurniawan/AFP

Rais wa UkraineVolodymyr Zelensky, mwezi uliopita aliandaa mkutano wa kilele wa amani nchini Uswisi kwa ajili ya kueleza mtazamo wake kuhusu amani ya kudumu. Urusi haikualikwa.

Soma Zaidi: Zelensky asema ataandaa mkutano mwingine wa kusaka amani 

China, mshirika wa karibu wa kisiasa na kiuchumi wa Urusi, haikuhudhuria mkutano huo wa kilele kwa sababu za kwamba mshirika wake Urusi haikualikwa.

Zelensky amesema nchi zenye nguvu duniani kama Marekani na China zinaweza kufaulu kuvimaliza vita kati ya nchi yake na Urusi.

Wakati huo huo Ukraine imefikia makubaliano ya awali na wadai wake juu ya kupanga upya ulipaji wa deni la bilioni 20 kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa. Hatua kama hiyo haijawahi kutokea katika nchi yoyote inayokumbwa na vita.

Kushoto: Rais wa Urusi Vladimir Putin. Kulia: Rais wa China Xi JinpingPicha: Sergei Guneev/Pool/Sputnik/REUTERS

Waziri wa Fedha wa Ukraine Serhiy Marchenko, amesema katika taarifa yake kwamba baada ya juhudi pamoja na wadai, shirika la fedha duniani IMF na washirika wa Ukraine wamefaulu kufikia makubaliano ya awali na Kamati ya Wadai ya Ad Hoc kuhusu marekebisho ya kina juu ya ulipaji wa madeni ya nje yanayoikabili Ukraine.

Serikali ya Ukraine imesemaIMF imethibitisha kuwa mpango huo unakwenda sambamba na vigezo vya kuisaidia nchi hiyo kwa kiasi cha dola bilioni 122 na kwamba wakopeshaji na wanaoidai Ukraine, pia wametia saini kukubaliana na mpango huo.

Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal, amesema mpango huo utaziweka huru rasilimali za Ukraine ili kukidhi mahitaji yake ya dharura, ya ulinzi wa usalama, ulinzi wa kijamii na kuufufua uchumi wa nchi hiyo.

Soma Zaidi:  Urusi: Ukraine kujiunga na NATO ni kutangaza vita

Kwingineko Shirika la ujasusi la Urusi, FSB, limesema limevikamata vilipuzi na nyenzo za vilipuzi vya umeme ambavyo vinaweza kutumika kufanya mashambulizi ya kigaidi. Vifaa hivyo vya kulipuka vimepatikana kwenye vifurushi huko St Petersburg na vilitoka Ujerumani na Italia.

Shirika hilo la ujasusi la Urusi limetangaza kuwa watu kadhaa wamekamatwa, lakini halikutoa maelezo zaidi.

FSB imesema imetoa taarifa kwa idara za ujasusi za Ulaya na imeomba msaada ili kuwabaini wahusika wakuu wa vitendo vya ugaidi wenye nia ya kuihujumu Urusi lakini maombi hayo hayajajibiwa bado.

Mnara wa Eiffel uliopambwa kwa nembo ya Michezo ya Olimpiki mjini Paris, Ufaransa.Picha: Tasos Katopodis/Getty Images

Na wakati ambapo mataifa yanakutana mjini Paris kushuhudia mashindano ya Olimpiki, Urusi haitawakilishwa kwa sababu imefukuzwa kwenye kushiriki mashindano hayo kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine na pia haitaruhusiwa kuitangaza michezo hiyo.

Vyanzo: AFP/DPA/RTRE