1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanadiplomasia maarufu duniani, Kissinger afariki dunia

1 Desemba 2023

Henry Kissinger, aliyekuwa mwanadiplomasia wa juu wa Marekani amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.

Henry Kissinger
Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Marekani Henry Kissinger.Picha: Brendan Smialowski/AFP

Pamoja na mambo mengine Kissinger anatajwa kuwa mtu aliyekuwa na ushiriki muhimu katika nyakati za vita vya Vietnam na kuimarisha uhusiano wa China na Marekani wakati akihudumu nafasi ya waziri wa mambo ya nje na mshauri wa usalama wa taifa lake.

Henry Kissinger, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel,mwaka 1973,  anayejulikana kwa mafanikio yake ya kidiplomasia na sera zenye utata, amefariki dunia Jumatano, akiwa na umri wa miaka 100. Taarifafa iliyotolewa imemtaja mwanasiasa huyo msomi wa Marekani na anaeheshimika kuwa ameaga dunia akiwa nyumbani kwako huko Connecticut.

Mazishi ya Kissinger yatafanywa ya kibinafsi na familia yake.

Aidha taarifa zinasema atazikwa katika kwa mazishi kibinafsi ya kifamilia, yatakayofuatiwa na ibada ya kumbukumbu ya umma itafanyika katika Jiji la New York. Viongozi wa ulimwengu kutoka katika pande tofauti za dunia wametoa salama za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe.

Kissinger anasifiwa kwa kuweka sawa uhusiano kati ya Marekani na China. Katika picha hii ya Machi 22, 1972, Kissinger akiwa mshauri wa taifa wa masuala ya usalama, kulia, alikutana na kiongozi wa China Mao Zedong mjini Beijing.Picha: XINHUA/AFP via Getty Images

Rais wa zamani George W. Bush amesema Marekani "imepoteza sauti moja ya kutegemewa na ya kipekee kuhusu masuala ya nje" huku Meya wa zamani wa Jiji la New York Michael Bloomberg akisema "Kissinger alikuwa mkarimu sana kwa hekima iliyopatikana katika maisha yake ya kipekee."

Ujerumani imeungana na ulimwengu katika maombolezo.

Kupitia mitandao ya kijamii kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amemtaja Kissinger kuwa mtu ambae ameiunda sera ya mambo ya nje ya Marekani kama ilivyokuwa kwa wengine wachache kadhaa. Kansela alikuwa akimsifu kwa namna alivyojitolewa katika kuimarisha urafiki kati ya Marekani na Ujerumani, akisema siku zote alijiweka karibu na taifa lake la asili-Ujerumani.

Kupitia ukurasa wake wa telegramu, Rais wa Urusi Vladimir Putin ametoa pole kwa mjane wa Kissinger, Nancy na akimtaja kiongozi huyo kuwa mtawala aliyekuwa na hekima na maono ya mbali.

China imemtaja Kissinger kuwa rafiki wa kweli wa raia wake.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin amezungumzia "umuhimu mkubwa kwa uhusiano wa China na Marekani" ulioambatanishwa na Kissinger na kuongeza kuwa Rais Xi Jinping ametuma ujumbe wa rambirambi kwa Rais wa Marekani Joe Biden. zaidi anasema "Dokta Kissinger ni rafiki wa muda mrefu na rafiki mkubwa wa watu wa China, na mwanzilishi na mjenzi wa uhusiano wa China na Marekani.

Hayati Henry Kissinger alipokutana na Rais wa China Xi Jinping mjini Peking Julai 20,2023Picha: China Daily/REUTERS

Kwa muda mrefu amejali na kuunga mkono maendeleo ya uhusiano kati ya China na Marekani, akiitembelea China zaidi ya mara mia moja na kutoa mchango wa kihistoria katika kukuza uhusiano wa kawaida kati ya China na Marekani. Watu wa China watakumbuka hisia za dhati za Dokta Kissinger na mchango muhimu katika uhusiano wa China na Marekani.”

Balozi wa China nchini Marekani,Xie Feng alisema "amesikitishwa sana" kwa taarifa ya kifo cha Kissinger akisema kifo hicho ni hasara kubwa kwa mataifa yao na dunia kwa ujumla.

Soma zaidi:Marekani imekua ikichukua njia mbalimbali za kukabiliana na ushawishi wa China unaozidi kuongezeka

Kissinger alizaliwa Ujerumani mwaka wa 1923. Familia yake ilihamia Marekani mwaka wa 1938 ili kukimbia utawala wa Kinazi. Alipata uraia wa Marekani mwaka 1943 na kulitumikia  Jeshi la Marekani wakati wa Vita Kuu ya II kwa upande wa Ulaya. Aliendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Harvard na kupata shahada ya uzamili 1952 na baadae shahada ya uzamivu 1954.

Chanzo: DW