Waziri wa Nje wa Libya asimamishwa kazi
28 Agosti 2023Waziri Mkuu wa Libya Abdul-Hamid Dbeibeh amemsimamisha kazi Waziri wake wa Mambo ya Nje, Najla Mangoush, kwa tuhuma za kukutana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Israel, Eli Cohen.
Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje ya Libya ilikanusha kwamba Najla Mangoush alifanya mkutano rasmi na Cohen, ikisema wawili hao walikutana katika mkutano usiokuwa rasmi mjini Rome, Italia.
Soma zaidi: Waziri wa mambo ya nje wa Libya asimamishwa kazi
Wizara hiyo ilisema inapinga kabisa uhalalishaji wowote wa mahusiano na Israel. Chini ya sheria ya Libya ya mwaka 1957, adhabu ya kushirikiana na Israel ni kifungo cha hadi miaka tisa jela.
Taarifa za kukutana mawaziri hao wa nje ilizuwa hasira kali nchini Libya, ambako kulishuhudiwa maandamano makubwa mjini Tripoli kupinga mkutano huo.
Hata hivyo, maafisa wa Israel waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba mkutano kati ya mawaziri hao ulikubaliwa kabla baina ya maafisa wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili.