1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa nje wa Marekani ziarani Berlin

26 Februari 2013

Waziri mpya wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, John Kerry, amewasili Berlin,kituo cha pili cha ziara yake ya siku 10 katika nchi za Ulaya ya Magharibi, Mashariki ya kati na katika Falme za kiarabu.

John Kerry akiwa mbele ya Lango la Brandenburg mjini BerlinPicha: Reuters

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, John Kerry, ataanza rasmi mazungumzo yake pamoja na waziri mwenzake Guido Westerwelle,saa nane mchana na baadaye amepangiwa kukutana na kansela Angela Merkel,kabla ya kuzungumza na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Serguei Lavrov, aliyekuja makusudi mjini Berlin  kwa ajili hiyo.

Mazungumzo hayo yatahusika miongoni mwa mengineyo na mipango ya kufikiwa makubaliano ya biashara huru kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Mada nyengine ni pamoja na mpango wa kuhamishwa vikosi vya kimataifa kutoka Afghanistan na mzozo wa Mashariki ya kati.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge la shirikisho inayoshughulikia siasa ya nje,Ruprecht Polenz,wa kutoka chama cha Christian Democratic Union,CDU,amesema anataraji ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,John Kerry,mjini Berlin itasaidia kuharakisha kutiwa saini makubaliano ya biashara huru kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya.

Marekani yahitaji Mshirika

Mwenyekiti wa kamati ya siasa ya nje ya bunge la shirikisho Ruprecht PolenzPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza na kituo cha Radio cha kusini mwa Ujerumani, Bayerisch Rundfunk, Ruprecht Polenz amesema anahisi enzi za Marekani kama dola pekee kuu linalodhamini usalama wa dunia,zimemalizika.Uongozi wa pamoja unaibuka na Marekani inahitaji mshirika, ameongeza kusema mwanasiasa huyo wa chama cha CDU aliyeitaja Ulaya kuwa "mshirika mkubwa wa Marekani kwa kuwa mabara yote mawili yana masilahi ya pamoja na yanafungamana kwa maadili ya aina moja.

Mada muhimu katika mazungumzo kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, John Kerry, na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, inahusu mzozo wa Syria, na mvutano uliozushwa na uamuzi wa serikali ya Urusi kupiga marufuku familia za Marekani zisiwalee watoto yatima wa kirusi.

Duru za kibalozi za Marekani zinasema waziri wa mambo ya nchi za nje John Kerry hategemei makubwa mwishoni mwa mazungumzo yake ya ana kwa ana pamoja na waziri mwenzake wa Urusi, Lavrow.

John Kerry ataondoka Berlin leo usiku kuelekea Paris, Ufaransa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

Mhariri: Josephat Charo