1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Baerbock akataa wazo la kuwapeleka wahamiaji Rwanda

18 Desemba 2023

Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani Annalena Baerbock amejitenga na pendekezo la kuwahamisha waomba hifadhi wa nchi yake kwenda Rwanda kama ilivyoamuwa serikali ya Uingereza.

Rwanda Kigali 2023 | Biontech | uazalishaji wa chanjo ya mRNA | Annalena Baerbock, Waziri wa mambo ya nje
Waziri Baerbock akihutubia mjini Kigali, Rwanda, wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza chanjo, Desemba 18, 2023.Picha: Florian Gaertner/photothek/picture alliance

Hayo ameyasema wakati akiwasili mjini Kigali kuhudhuria uzinduzi wa kiwanda cha madawa ya chanjo za maradhi ya maambukizo huku akiahidi kuwa yake itafanya kila iwezekenalo kusaidia utengenezaji wa chanjo barani Afrika.

Wakati wa ziara yake iliyoanza leo kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki, ambako kampuni ya chanjo ya Ujerumani BioNTech ilitarajiwa kufungua kiwanda cha kwanza cha kutengeneza chanjo, Annalena Baerbock amegusia masuala kadhaa ambayo yamekuwa yakigonga vichwa vya habari, ukiwemo mjadala wa kuwahamisha wahamiaji kuwapeleka Rwanda.

Amejitenga na pendekezo hilo lililotaja Ghana au nchi nyingine zisizokuwa za mashariki mwa Umoja wa Ulaya kwamba wahamiaji walioingia Ulaya wanaweza kuhamishwa.

Soma pia: Baerbock anasema kiwanda cha chanjo nchini Rwanda ni hatua muhimu

Bearbock "alishangazwa" kwamba "wanasiasa wa kihafidhina hasa" walikuwa wakitoa wito kwa watu wanaokimbilia Ulaya kuletwa katika nchi kama vile Rwanda.

Amesema mawazo hayo yanalenga kubatilisha mjadala kutoka kwenye lengo halisi ambalo ni utekelezaji wa sera ya pamoja ya hifadhi ya Umoja wa Ulaya.

Waziri Baerbock akiwasikiliza wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza chanjo ya mRNA, kilichozinduliwa Kigali, Rwanda, Desemba 18, 2023.Picha: Florian Gaertner/photothek/picture alliance

Makubaliano kama hayo ambayo yamekuwa yakigonga vichwa vya habari siku za hivi karibuni kati ya Uingereza na Rwanda, yanatoa fursa kwa watu wanaowasili Uingereza kupelekwa Rwanda, bila maombi yao ya hifadhi kuchunguzwa. Wazo ambalo licha ya kupingwa na mahakama ya juu Uingereza, waziri wake mkuu Rishi Sunak angali anajaribu mbinu za kuhakikisha linafanikiwa.

Ujerumani kuisadia bara la Afrika kutengeneza chanjo

Kuhusu ushirikiano na bara la Afrika, Baerbock amesema bara la Afrika litapata msaada kikamilifu kutoka Ujerumani na Umoja wa Ulaya, katika vita dhidi ya majanga na maradhi.

Maneno yake yamejiri mnamo wakati kampuni ya kutengeneza dawa ya BioNTech ikifungua kiwanda cha kutengeneza chanjo aina ya mRNA kusambaza dozi barani Afrika endapo kutatokea majanga mengine siku zijazo kama COVID-19.

Soma pia: Baerbock ziarani Rwanda kushuhudia uzinduzi wa kiwanda cha chanjo

Kiwanda hicho cha BioNTech kinatarajiwa kuanza kutengeneza chanjo mwaka 2025 na kitawaajiri wafanyakazi 100 mjini Kigali.Aidha- kampuni hiyo yenye makao yake makuu mjini Mainz imesema imekadiria uwekezaji huo kuwa wa thamani ya takriban dola milioni 150.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock (kushoto) akifuatilia uzindizi wa kiwanda cha Biontech cha uzalishaji wa chanzo ya mRNA mjini Kigali, Desemba 18, 2023.Picha: Florian Gaertner/photothek/picture alliance

Kuna uwezekano wa chanjo nyingine kama dhidi ya malaria na kifua kikuu kutengenezwa kwenye kiwanda hicho katika siku zijazo, ikiwa idhini itatolewa.

Kulingana na Wizara ya Maendeleo ya Ujerumani, serikali ya Berlin inaunga mkono uanzishwaji wa chanjo endelevu na uzalishaji wa dawa barani Afrika ili kusaidia kutayarisha bara hilo kuyakabili magonjwa katika siku zijazo.

Ujerumani inachangia zaidi ya euro milioni 550, ambapo karibu milioni 500 inatokana na ushirikiano wa kimaendeleo kati yake na Afrika. Lengo likiwa ni kuwezesha Afrika la kutengeneza hadi asilimia 60 ya chanjo zinazotumika ndani ya bara hilo ifikapo mwaka 2040.

Usaidizi mwingine unaoitolewa na Ujerumani ni mafunzo kwa wataalam, kuanzishwa kwa mamlaka za kitaifa za udhibiti na kuwekwa kwa taratibu za kuvutia biashara.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW