1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gabriel afanya ziara ya kihistoria Iran

19 Julai 2015

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Simar Gabriel amekwenda Iran Jumapili (19.07.2015) akiwa ni kiongozi wa kwanza mwandamizi wa mataifa ya magharibi kuitembelea nchi hiyo tokea kufikiwa makubaliano ya kihistoria ya nyuklia.

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tehran. (19.07.2015)
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tehran. (19.07.2015)Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

.Gabriel ambaye pia ni naibu kansela na waziri wa nishati ameanza ziara yake hiyo ya siku tatu akiandamana na ujummbe mdogo wa wawakilishi kutoka makampuni, mashirika ya nishati na taasisi nyengine za kisayansi.

Gabriel anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais Hassan Rouhani wa Iran na mawaziri kadhaa kufuatia makubaliano ya nyuklia ya kihistoria yaliofikiwa Jumanne.

Waziri huyo amesema katika taarifa kwamba makubaliano hayo yaliokuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu yameweka msingi wa kurudisha tena katika hali ya kawaida uhusiano wa kiuchumi na Iran kwa sharti kwamba hatua zilizotajwa katika makubaliano hayo hivi sasa zinatekelezwa.

Ishara ya kutia moyo

Mkuu wa chama cha Wafanyabiashara na Viwanda nchini Ujerumani Eric Schweiter ambaye anaandamana na Gabriel katika ziara hiyo ameiita ziara hiyo kuwa ni ishara ya kutia moyo kwa makampuni ambayo yalikuwa yamepigwa marufuku kufanya biashara na nchi hiyo ya Ghuba yenye utajiri wa rasilmali kutokana na vikwazo ilivyowekewa na mataifa ya magharibi.

Waziiri wa uchumi wa Ujerumani Simar Gabriel katikati akipokewa na naibu waziri wa mafuta wa Iran Hossein Zamaninia (kulia) uwanja wa ndege wa Tehran. (19.07.2015)Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Schweitzer ametaka kampuni za Ujerumani zipewe kinga ya kisheria kwa uwekezaji watakaouweka nchini Iran iwapo serikali ya nchi hiyo itakiuka masharti ya makubaliano ya nyuklia na kuwekewa tena vikwazo vya kibiashara.

Ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa mfumo wa aina hiyo utazipa kampuni za Kijerumani ulinzi wa kisheria unaohitajika kuzifanya zirejee Iran.

Washirika wa biashara

Ujerumani na Iran kihistoria zilikuwa washirika wa karibu wa biashara lakini biashara kati yao imeshuka kutokana na nchi hiyo kuwekewa vikwazo ambapo hapo mwaka jana imeshuka hadi kufikia euro bilioni 2.4 kutoka euro bilioni nane kwa mwaka 2003-2004.

Waziiri wa uchumi wa Ujerumani Simar Gabriel (kulia) na naibu waziri wa mafuta wa Iran Hossein Zamaninia Tehran.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Viongozi wa kibiashara wa Ujerumani wametaka kukidhi mahitaji ya kufanya miundo mbinu ya viwanda nchini Iran kuwa ya kisasa hususan katika sekta ya mafuta kutokana na kwamba ina fursa nyingi za faida.Kampuni za uhandisi,kemikali, madawa,vipuri vya magari na reli zote zinatarajia kujipatia kandarasi kubwa.

Iran inashika nafasi ya nne kwa kuwa na akiba kubwa kabisa ya mafuta duniani na nafasi ya pili kwa akiba ya gesi jambo ambalo linaamisha ina akiba kubwa kabisa ya nishati rasilmali hizo zikichangaywa pamoja.

Wizara ya mafuta ya Iran imetangaza kwamba inakusudia kuvutia uwekezaji wa kigeni unaofikia thamani ya dola bilioni 100 kuifanya sekta hiyo kuwa ya kisasa ambayo haikuendelezwa kwa muongo mzima.

Suala la haki za binaadamu lakumbushwa

Hata hivyo wakosoaji wa Iran wamemtaka Gabriel asilifumbie macho suala la haki za binaadamu katika kinyan'ganyiro cha kuwania kujenga upya uhusiano wa kibiashara.

Christian Mihr Mkuu wa Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka Tawi la Ujerumani.Picha: DW

Mjomba wa Reyahaneh Jabbari raia wa Iran mwenye umri wa miaka 26 aliyenyongwa mwaka jana kwa kumuuwa afisa wa ujasusi wa zamani kwa kile alichosema kujihami asimbake ameliambia gazeti la Ujerumani la Bild kwamba Gabriel anafanya biashara na utawala wa kinyama.

Fariborz Jabbari ambaye anaishi Berlin amekaririwa akisema "wakati anaposaini mikataba akumbuke watu waosota magerezani,wakosoaji wa utawala huo watu wanaoteswa na kutiwa hatiani."

Kiongozi wa Shirika la Waandishi wa habari wasiokuwa na mipala tawi la Ujerumani Christina Mihr ameliambia gazeti la Bild itakuwa "balaa" iwapo ziara ya Gabriel itaweka mbele suala la biashara ya kiuchumi kuliko la haki za binaadamu na uhuru wa vyombo vya habari.

Makubaliano ya kimataifa yaliofikiwa Vienna yanakusudia kuhakikisha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijipatii silaha za nyuklia.Badala yake nchi hiyo itaregezewa hatua kwa hatua vikwazo vya kimataifa vilivyoiathri vibaya nchi hiyo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Yusra Buwayhid