Waziri wa Ufaransa; Argentina 'washindi wasio na heshima'
23 Desemba 2022Video zilizopigwa wakati wa sherehe za Kombe la Dunia zikionyesha ubaguzi wa rangi dhidi ya mshambuliaji wa timu ya taifa ya kandanda ya Ufaransa Kylian Mbappe zimekuwa zikienea kwenye mitandao ya kijamii na kuibua hasira haswa nchini Ufaransa.
soma Maoni: Messi ndie bora zaidi kombe la Dunia 2022
Katika video moja, baadhi ya mashabiki wa Argentina walishangilia wakiwa wamebeba bango lenye umbo la jeneza linaloonyesha sura ya nyota wa Ufaransa Kylian Mbappe likiungua. Katika video nyingine, shabiki wa Argentina anaonekana akiwa ameshikilia juu hewani mwanasesere aliyefunikwa kwa karatasi nyeusi iliyoandikwa "Mbappe".
soma Timu ya Argentina yarejea nyumbani kutoka Qatar
Waziri wa michezo wa Ufaransa Amélie Oudéa-Castéra amewashutumu wachezaji wa timu ya taifa ya kandanda ya Argentina na kuwataja kama "washindi wasio na heshima" na "wachafu" kwa kumkejeli nyota wa nchi yake Kylian Mbappe baada ya kushinda fainali ya Kombe la Dunia.
"Kwa jinsi timu yetu ya Ufaransa ilivyopoteza kwa ujasiri, na jinsi timu hii ya Argentina ilivyofanya baada ya ushindi huu haikustahili mechi tuliyoona", waziri Oudéa-Castéra alikiambia kituo cha redio cha Ufaransa RTL.
Oudéa-Castéra alimtaja mlinda mlango Emiliano Martinez, ambaye alionekana kwenye gwaride la ushindi mjini Buenos Aires akiwa ameshikilia mwanasesere uso wake ukiwa umefunikwa na picha ya nyota wa Ufaransa Mbappe.
soma Argentina yanyakua ubingwa
Baada ya ushindi
Mara tu baada ya mechi, mwito wa "ukimya wa dakika moja... kwa Mbappe," ulisikika kutoka kwa chumba cha kubadilishia nguo cha Argentina.
Mbappe alifunga 'hat-trick' wakati Ufaransa ikipambana mara mbili na kusawazisha mechi hiyo iliyoishia kwa mikwaju ya penalti.
"Naona inasikitisha," Oudea-Castera alisema. "Ni uchafu tu, haifai, kwa kweli sio kwa hafla hiyo," alisema. "Huyu Emiliano Martinez hajitofautishi. Inasikitisha".
Waziri huyo alisema alifurahishwa na kwamba rais wa Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) Noel Le Graet alimwandikia mwenzake wa Argentina kulalamika kuhusu "kukithiri kwa njia isiyo ya kawaida" katika sherehe hizo.
FFF pia imesema inakusudia kuwasilisha malalamiko dhidi ya mashabiki wa Ufaransa ambao walichapisha maoni ya ubaguzi wa rangi kwenye mitandao ya kijamii baada ya Kingsley Coman na Aurelien Tchouameni kukosa mkwaju wa penalti.
AFPE/ DW