Jim Mattis awasiliwa Afghanistan
13 Machi 2018Mattis aliyasema hayo muda mfupi baada ya kuwasili Kabul, ambako kuna wasiwasi wa usalama kiasi kuwa wanahabari wanaosafiri naye hawakuruhusiwa kuchapisha habari zao hadi kikundi chake kilipoondoka katika uwanja wa ndege wa Kabul na kufika kwenye makao makuu ya kikosi cha muungano kinachoongozwa na Marekani.
Waandishi wa habari wazuiwa kuchapisha habari
Tukio la waandishi habari kuzuiwa kuchapisha habari zao ni la kwanza kutokea katika historia ya ziara kama hiyo nchini humo.
Mattis amesema, tunatazamia ushindi nchini Afghanistan," ameongeza kusema, "sio ushindi wa kijeshi lakini wa upatanisho wa kisiasa na wataliban ambao umesababisha mkwamo katika miaka ya hivi karibuni."
Mattis ambaye ni jenerali mkuu mstaafu wa vikosi vya jeshi la wanamaji aliyeliongoza jeshi la Marekani Kusini mwa Afghanistan katika hatua ya kwanza ya vita mwaka 2001 alisema, "kuwapatanisha Watalibani ni hatua ya daraja ndefu."
Ameelezea ushindi wa Afghanistan kuwa suluhisho kati ya serikali na Wataliban ambalo huenda likaliunganisha taifa hilo. Aliongeza kusema kuwa iwapo hayo yatafikiwa taifa la Afghanistan halitakuwa kituo cha mashambulio ya kimataifa kama ilivyokuwa wakati kundi la kigaidi la al-Qaida lilipolitumia taifa hilo kuishambulia Marekani Septemba, 11 mwaka 2001.
Wataliban wanataka mazungumzo yafanyike Washington
Ziara ya Mattis ni ya pili tangu rais Donald Trump kutangaza mwezi Agosti mwaka uliopita kuwa licha ya kutaka kuwaondoa wanajeshi wa Marekani ambao wamekuwa nchini humo kwa miaka 17, utawala wake utachukua mtazamo mwengine wa kutatua matatizo ya taifa hilo.
Hata hivyo waasi wa Taliban wanashiikilia kuwa ili kuwe na mazungumzo na upende wa serikali, lazima yafanyikie Washington, Marekani.
Profesa Stephen Biddle, mtaalamu wa msuala ya siasa katika chuo kikuu cha George Washington na mwangalizi wa muda mrefu wa mzozo wa Afghanistan amesema, "nina Imani kuwa mkakati wa Marekani utaleta tofauti na matumaini kwa mchakato wa kusuluhisha tofauti zilizopo."
Kiongozi wa Taliban na rais Ashraf Ghani wamefanya mazungumzo ya kuwapatanisha katika siku za hivi karibuni. Mwisho wa mwezi Februari rais Ghani aliwashirikisha Wataliban kwenye kongamano la amani la kuokoa taifa hilo.
Afisa mkuu wa Marekani katika wizara ya ulinzi Alice Wells, Ijumaa iliyopita katika Taasisi ya Amani nchini humo, alisema, "mtazamo wa rais Ghani tafauti na siku za nyuma ni wa kujumuisha kila mmoja, katika kupata suluhisho la mgogoro wa nchi hiyo."
Hata hivyo mashirika ya usalama ya Marekani yana matumaini madogo ya kuwepo kwa mafanikio 2018 katika uwanja wa vita.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman