Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis kujiuzulu
21 Desemba 2018Uamuzi huo wa Mattis ulitarajiwa baada ya tangazo la Rais Trump la kuondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria, hatua ambayo imewakasirisha washauri wake na washirika wa Marekani.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Jim Mattis amesema anaamini kwa dhati kwamba Marekani inahitaji kuendeleza ushirikiano imara na washirika wake, na kwamba inapaswa kuweka msimamo usio na utata dhidi ya mataifa kama China na Urusi.
Jenerali huyo mstaafu pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mpangilio wa namna dunia inavyoongozwa, ambao amesema unasimamia vyema maslahi ya Marekani kiusalama, kiuchumi na kimaadili.
Mtazamo tofauti na mkubwa
Ameweka wazi kwamba mtazamo wake huo unatofautiana na ule wa Rais Donald Trump, na hivyo kuondoka kwake kunatoa fursa ya kuteuliwa waziri mpya wa ulinzi ambaye ana maoni sawa na rais.
Trump amesema atatangaza mrithi wa Mattis haraka iwezekanavyo.
Kulingana na takwimu za taasisi ya Brookings, utawala wa Trump tayari unaongoza kwa kubadilishabadilisha maafisa wa ngazi za juu, ukilinganishwa na wa marais watano kabla yake.
Wanasiasa watoa kauli zao
Wanasiasa wa ngazi za juu nchini Marekani, wakiwemo kutoka chama cha Republican cha Trump wamesikitishwa na kuondoka kwa Mattis. Mbunge Lindsey Graham wa Republican amesema kuondoka kwa waziri huyo kumeondoa sauti ambayo Rais Trump alipaswa kuisikiliza.
Mmoja wa vinara wa chama cha Democratic Nancy Pelosi, amesema imedhihirika kwamba utawala wa Trump umeyapa kisogo maadili ya msingi kwa Marekani, akisema busara na uzoefu vya Jim Mattis vinaacha pengo katika wizara ya ulinzi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, rtre
Mhariri: Grace Kabogo