Waziri wa ulinzi wa Ujerumani afanya ziara ya kushtukiza Afghanistan
14 Aprili 2010Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya ulinzi ya Ujerumani mjini Berlin, waziri Karl-Theodor zu Guttenberg, ameyatembelea makao makuu ya kikosi cha Ujerumani chenye wanajeshi 4,500 huko Mazar-i-Scharif kaskazini mwa Afghanistan kabla kuelekea katika mji wa Kunduz. Akizungumza katika kambi hiyo, waziri huyo amesema na hapa namnukulu, "Kwangu mimi ni muhimu kuwafafanulia wazi wanajeshi wetu walio Aghanistan kwamba viongozi wa kisiasa wa ngazi ya juu wanawaunga mkono na wako nyuma yao," mwisho wa kumnukulu waziri Karl- Thedor zu Guttenberg.
Ziara ya waziri huyo nchini Afghanistan inalenga kuuelezea umma wa Ujerumani maana ya kazi waliyonayo wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan. Kiongozi huyo amesisitiza haja ya kutowasahau wanajeshi wa Ujerumani badala yake kuwasaidia.
Kufuatia kuuwawa kwa wanajeshi watatu wa Ujerumani siku ya Ijumaa Kuu mwaka huu, katika mkoa wa Kunduz, umaarufu wa tume ya Ujerumani nchini Afghanistan umepungua zaidi. Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Forsa, yaliyochapishwa leo na jarida la Stern la hapa Ujerumani, asilimia 62 ya Wajerumani wanaunga mkono kuondoka wanajeshi wa Ujerumani kutoka nchini Afghanistan. Hiki kinaelezwa kuwa kiwango kikubwa kuwahi kufikiwa katika tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo ya Forsa kuhusu kuwepo kwa wanajeshi wa Ujerumani huko Afghanistan.
Katika ziara yake hiyo ambayo haikutangazwa kutokana na sababu za kiusalama, waziri Karl- Theodor zu Guttenberg, anataka kupata taarifa zaidi kuhusu mashambulio ya hivi karibuni ya wapiganaji wa kundi la Taliban dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani. Amesema, "Kuna ulazima wa kuchunguza uwezekano wa kuboresha vifaa walivyonavyo wanajeshi mahali waliko, na ili kuweza kufanya hivyo ni vyema kulitembelea eneo la tukio."
Kwa heshima ya wanajeshi watatu wa Ujerumani waliouwawa siku ya Ijumaa Kuu, waziri Karl- Theodor zu Guttenberg, atazindua jiwe la ukumbusho lenye majina ya wanajeshi hao. Amewashukuru wanajeshi wa Ujerumani kwa juhudi zao nchini Afghanistan.
Akiwa nchini Afghanistan, waziri Karl- Theodor zu Guttenberg ametupilia mbali mwito wa chama cha Social Democratic, SPD, kutaka mamlaka mpya ya bunge la Ujerumani, Bundestag, kuhusu tume ya jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan. Amesema mamlaka ya sasa iliyotolewa na bunge inaelezea kinagaubaga kuhusu hali halisi.
Kiongozi wa chama cha SPD, Sigmar Gabriel, aliliambia gazeti la Frankfurter Allgemeine siku ya Jumanne wiki hii kwamba ikiwa serikali ya Ujerumani inaiona tume ya Ujerumani iko katika hali ya vita nchini Afghanistan, basi inalazimka kwanza kupata kibali kipya.
Ziara ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani Karl Theodor zu Guttenberg nchini Afghanistan, inafanyika huku kamanda mkuu wa jeshi la Marekani, anayeongoza kikosi cha NATO, jenerali Stanley McCrystal, akitarajiwa kufanya ziara ya siku tatu nchini Ujerumani kuanzia Jumatatu wiki ijayo.
Mwandishi: Josephat Charo/DPA
Mhariri: Abdul-Rahman