1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani aizuru Kiev

14 Januari 2025

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amewasili mjini Kiev, Ukraine kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa serikali ya nchi hiyo kujadiliana kuhusu utoaji wa misaada zaidi na kutathmini hali ya kijeshi.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris PistoriusPicha: dts Nachrichtenagentur(IMAGO

Pistorius ambaye amewasili Jumanne asubuhi mjini Kiev, amesema kupitia ziara yake hiyo ni muhimu kuonyesha kuwa wanaendelea kuiunga mkono Ukraine kikamilifu. Kulingana na shirika la habari la Ujerumani, DPA, Pistorius atafanya mikutano itakayoangazia suala la kuendeleza ushirikiano na misaada katika sekta ya ulinzi ya Ukraine.

Akizungumza baada ya kuwasili Kiev, Pistorius amesema ni ishara kwamba Ujerumani, kama nchi kubwa zaidi katika Jumuia ya Kujihami ya NATO barani Ulaya, inasimama na Ukraine. Sio peke yake, bali na Kundi la Mataifa Matano na washirika wengine wengi.

Majadiliano kuhusu upelekaji silaha Ukraine

Ziara ya Pistorius inafanyika siku moja baada ya siku ya Jumatatu kuizuru Warsaw, ambako alikutana na mawaziri wenzake wa Poland, Ufaransa, Uingereza na Italia, na walijadiliana kuhusu upelekaji wa silaha kwa Ukraine.

Akiwa Poland, Pistorius amesema kama pesa zipo, kama uwezo wa kuzalisha silaha upo, basi Ukraine yenyewe itaharakisha kuwapa wanajeshi wake nyenzo na silaha. ''Pamoja na upelekaji wa vifaa, kuimarisha sekta ya ulinzi ya Ukraine ni kigezo muhimu ambacho tunakizingatia. Lazima tukiimarishe kwa kufadhili miradi ya manunuzi ya Ukraine, na hilo ni jambo muhimu sana,'' alifafanua Pistorius.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius akiwa na mawaziri wenzake kutoka Poland, Ufaransa, Uingereza na Italia.Picha: Aleksandra Szmigiel/REUTERS

Aidha, wiki iliyopita, Pistorius alikutana na waziri mwenzake wa Ukraine katika mkutano wa kundi la mataifa yanayoiunga mkono Ukraine, kwenye kambi ya jeshi la Marekani ya Ramstein iliyoko nchini Ujerumani.

Ziara ya Pistorius inafanyika wiki moja kabla ya kuapishwa kwa rais mteule wa Marekani, Donald Trump. Sera ya Marekani kuelekea Ukraine inatarajiwa kubadilika kwa kiasi kikubwa chini ya utawala wa Trump. Ukraine ina wasiwasi kuwa Trump ataishinikiza nchi hiyo kufikia makubaliano na Urusi, na kabla ya kuapishwa kwake maafisa wa Ukraine wamekuwa wakizidisha mawasiliano na wenzao wa Ulaya.

Ujerumani ya pili kwa kuipatia Ukraine misaada

Ujerumani imekuwa nchi ya pili ambayo inatoa misaada ya kijeshi kwa Ukraine, baada ya Marekani, katika vita vyake dhidi ya Urusi, lakini kumekuwepo na mijadala ya mara kwa mara ndani ya Ujerumani kuhusu kiwango cha misaada hiyo.

Wakati huo huo, jeshi la anga la Ukraine limesema limezidungua droni 58 kati ya 80 zilizorushwa na Urusi kwenye maeneo 11 ya Ukraine usiku wa kuamkia Jumanne. Taarifa iliyotolea Jumanne na jeshi la anga imeeleza kuwa droni 21 zilitoweka kwenye rada, kutokana na mifumo ya kielektroniki inayotumiwa na Ukraine kuzielekeza. Kulingana na jeshi hilo, Urusi pia imeishambulia Ukraine kwa makombora matano yaliyotengenezwa na Marekani aina ya ATACMS.

(AFP, DPA, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW