Waziri wa Uturuki akutana na maafisa wa Hamas Istanbul
1 Novemba 2025
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan amekutana hii leo na maafisa wa tawi la kisiasa la kundi la wanamgambo wa Kipalestina Hamas mjini Istanbul, kwa mujibu wa shirika la utangazaji la umma la nchi hiyo,TRT. Mkutano huo unafanyika kuelekea mazungumzo yaliyopangwa Jumatatu baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi kadhaa za Kiislamu kujadili usitishaji vita Gaza na uwezekano wa hatua zinazofuata.
Kwa mujibu wa Fidan, mkutano huo utawaleta pamoja mawaziri kutoka mataifa nane ambayo yalikutana na Rais Donald Trump mjini New York mnamo mwezi Septemba. Mazungumzo hayo yatajikita namna ya kuendelea na awamu ya pili ya mpango wa kusitisha vita. Suala kubwa katika awamu hiyo ni kuanzishwa kwa kikosi cha kimataifa cha kuleta utulivu huko Gaza.