Waziri Westerwelle ziarani Mali
1 Novemba 2012Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle yuko ziarani katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika wakati ambapo juhudi za kimataifa zimeshika kasi kuandaa opereshini za kijeshi kulikomboa eneo la kaskazini la Mali. Mwanadiplomasia huyo wa kutoka chama cha kiliberali cha FDP amewasili Bamako leo asubuhi akitokea nchi jirani ya Senegal.Amepanga kuzungumza na viongozi wa utawala wa mpito wa Mali pamoja pia na wabunge kutoka eneo la mzozo la kaskazini.
"Tunasimama bega kwa bega na wananchi wa Mali katika kusaka ufumbuzi wa mzozo wa kaskazini amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa ujerumani na kuongeza"Ujerumani haitoipatia mali silaha na wala haitatuma wanajeshi.Tutasadia katika kutoa mafunzo,tutatoa misaada ya kiufundi,ya fedha na ya kiutu kwaajili ya tume ya nchi za kiafrika."
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani amekumbusha magaidi wakijipatia uwanja kusini mwa jangwa la Sahara,hali hiyo itahatarisha pia usalama upande wa pili wa bahari ya kati.
Wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam wametumia vurugu ya baada ya mapinduzi ya kijeshi,mwezi March uliopita,kudhibiti thuluthi mbili ya eneo la kaskazini la Mali.Wataalam kutoka shirika la kiuchumi la nchi za Afrika Magharibi-ECOWAS,Umoja wa Afrika,Umoja wa ulaya na Umoja wa mataifa wanakutana tangu jumanne iliyopita mjini Bamako kuandaa mpango madhubuti utakaowasilishwa mbele ya Umoja wa mataifa hadi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa November.Wataalam hao wataendelea na mazungumzo yao hadi jumapili ijayo.
Umoja wa Ulaya unapanga kutoa vifaa na mafunzo kwa vikosi vya serikali ya Mali pia kusaidia mpango huo wa kulikomboa eneo la kaskazini la nchi hiyo.
Ziara hii fupi ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle imelengwa zaidi kuhimiza juhudi za kisiasa pia kuumaliza mzozo wa Mali.Guido Westerwelle ametoa mwito wa kuendelezwa mazungumzo na pande zote zenye nia ya kusaka ufumbuzi wa mzozo wa kaskazini.
Hatua kali za usalama zimechukuliwa nchini Mali mnamo wakati huu wa ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani mjini Bamako-ziara iliyowekwa siri hadi atakapoondoka.Guido Westerwelle ameanza ziara yake ya Afrika jana kwa kuitembelea Senegal,.Kkesho atakwenda Nigeria anakopanga kusalia hadi jumamosi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef