WEF: Je, Greenland ndiyo kengele ya uamsho kwa Ulaya?
21 Januari 2026
Mkutano wa mwaka huu wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos ulikuwa umetabiriwa mapema kuwa ungegubikwa na jina la Donald Trump. Rais huyo wa Marekani, anayerejea Davos baada ya miaka sita, amechangia pakubwa kuyumba kwa mpangilio wa dunia—hali ambayo washiriki wa mkutano wa siku tano wanajaribu kuitafakari na kuijadili.
Lakini hatua ya Trump kutishia kutoza ushuru baadhi ya washirika wa karibu wa Marekani ili kuwashinikiza kuunga mkono mpango wake wa kuitwaa Greenland kutoka Denmark, nchi mwanachama wa NATO, imeongeza mvutano kwa kiwango kipya kabisa.
Kwa viongozi wa Ulaya wanaowasili katika mji wa milimani wa Uswisi, tishio hilo ni pigo jingine kubwa kwa uhusiano wa kihistoria kati ya Ulaya na Marekani, ambao tayari ulikuwa umelegea.
Umoja wa Ulaya haujakaa kimya. Umejibu kwa msimamo mkali, ukiandaa hatua za kiuchumi za kulipiza kisasi dhidi ya makampuni ya Marekani na kujadili matumizi ya chombo chake maalum cha kupinga shinikizo la kiuchumi (Anti-Coercion Instrument – ACI), ambacho kinaweza kuzuia au kupunguza ushiriki wa kampuni za Marekani katika soko kubwa la pamoja la EU.
Tukio hilo limekazia tena haja ya Ulaya kuacha hali ya kuridhika na hali ilivyo na kutathmini upya utegemezi wake kwa Marekani katika nyanja nyingi, kuanzia ulinzi hadi teknolojia. Hili pia limekuwa mada muhimu ya majadiliano katika mkutano wa WEF.
Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, aliwaambia washiriki wa WEF kuwa "mabadiliko makubwa” yanayoikumba Ulaya kwa sasa ni "fursa,” na kwa hakika ni "hitaji la lazima la kujenga aina mpya ya uhuru wa Ulaya.”
Aliongeza kuwa Ulaya itaweza kunufaika na fursa hiyo endapo tu itakubali kuwa mabadiliko hayo si ya muda mfupi, bali ni ya kudumu.
Fursa kwa Ulaya
Hadi sasa, viongozi wa Umoja wa Ulaya wamejaribu kumzuia Trump asigeuze migogoro ya kibiashara na kidiplomasia kuwa mpasuko mkubwa kabisa katika uhusiano wa Marekani na Ulaya. Lakini juhudi hizo zimeigharimu Ulaya kisiasa na kiuchumi.
Kwa mfano, licha ya kuwa wafadhili wakubwa zaidi wa kijeshi na kifedha wa Kyiv, nchi za Ulaya zilitengwa katika mazungumzo ya amani kuhusu Ukraine. Aidha, zilikubali mkataba wa kibiashara na Marekani ambao wengi wanaona haukuwa na uwiano wa haki.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa Ulaya inapaswa kuwa thabiti zaidi inaposhughulika na Marekani, ikizingatiwa nguvu kubwa iliyo nayo. Ulaya si tu soko kubwa kwa makampuni ya Marekani, bali pia ndiyo mkopeshaji mkubwa zaidi wa Marekani, ikimiliki dhamana na hisa za Marekani zenye thamani ya matrilioni ya dola—karibu mara mbili ya kiasi kinachomilikiwa na dunia nzima iliyobaki.
Hili ni jambo nyeti, hasa ikizingatiwa jinsi Marekani inavyotegemea madeni kugharamia matumizi yake ya kila siku.
Wataalamu hao wanataja mfano wa China, ambayo ilitumia udhibiti wake wa madini adimu kumlazimisha Trump kupunguza ushuru mkubwa aliokuwa ameiwekea. Ingawa kuuza dhamana za Marekani si jambo rahisi, Umoja wa Ulaya tayari unaangalia hatua ambazo zinaweza kuyafanya maisha kuwa magumu kwa makampuni ya Marekani yanayofanya biashara ndani ya soko la Ulaya.
Hata hivyo, wapo wengine wanaokubaliana na von der Leyen kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kutumia fursa hii kukabiliana na changamoto zake za muda mrefu, huku ukiendelea kushughulikia mvutano unaoongezeka na Marekani kwa muda mfupi.
"Kadri unavyoongeza uzalishaji wako, ndivyo unavyokuwa na ushindani zaidi, na ndivyo unavyopata nguvu zaidi katika ulingo wa kimataifa,” alisema Matthias Tauber, mkuu wa shughuli za Ulaya katika Taasisi ya Boston Consulting Group, katika mahojiano na DW.
"Maendeleo ya hivi karibuni yanaonyesha wazi jinsi uzalishaji na ushindani ulivyo muhimu. Hapa ndipo Ulaya inapaswa kuongeza kasi na kufanya vizuri zaidi.”
Uchumi unaodorora na ushindani uliopotea
Uchumi wa Ulaya umekuwa ukikua kwa kasi ndogo na ya kusuasua kwa miaka kadhaa sasa, ukizuiwa na matatizo ya kimuundo yaliyojikita kwa kina. Miongoni mwa matatizo hayo ni ucheleweshaji wa maamuzi unaosababishwa na mfumo tata wa uongozi, kanuni zisizo na unyumbufu wa kutosha, ukosefu wa uhakika wa nishati, pamoja na utegemezi mkubwa wa uagizaji wa malighafi muhimu kutoka nje.
Baadhi ya changamoto hizi zimeifanya Ulaya izidi kubaki nyuma ya Marekani katika ukuaji wa uchumi, ongezeko la kipato cha matumizi, na tija ya kazi, hali inayopunguza mvuto wake kwa wawekezaji. Kampuni nyingi za Ulaya—hasa zile changa—zimekuwa na ugumu wa kupata mitaji kwa sababu masoko ya fedha barani humo ni madogo na yamegawanyika.
Changamoto hizi si mpya. Zilibainishwa pia katika ripoti ya mwaka 2024 kuhusu ushindani wa Ulaya iliyoandaliwa na aliyekuwa rais wa Benki Kuu ya Ulaya (ECB), Mario Draghi. Hata hivyo, zaidi ya mwaka mmoja baadaye, hatua chache sana zimechukuliwa kutekeleza mapendekezo yake.
Ursula von der Leyen alizigusia changamoto hizo katika hotuba yake huko Davos, akisisitiza hasa umuhimu wa kuunda mazingira ya kisheria yaliyo rahisi zaidi na yanayotabirika. "Tunaishi katika zama ambazo mtaji au data vinaweza kuvuka Ulaya ndani ya sekunde moja,” alisema. "Na biashara pia lazima iweze kusogea kwa uhuru huo huo.”
Kupunguza hatari na utegemezi wa Marekani
Mabadiliko ya mpangilio wa dunia aliyoyataja von der Leyen tayari yameibua hali ya uharaka ndani ya Umoja wa Ulaya. Hili linaonekana kupitia kutiwa saini kwa mkataba mkubwa wa biashara huria na jumuiya ya Mercosur ya Amerika Kusini baada ya miaka 25 ya mazungumzo, pamoja na mkataba mwingine unaotarajiwa kusainiwa na India.
Wakati huo huo, EU inawekeza kwa kiwango kikubwa katika ulinzi—mamia ya mabilioni ya euro kwa pamoja—ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza utegemezi wake kwa nchi zisizo wanachama wa EU, ikiwemo Marekani.
Kuna utegemezi mwingine ambao EU inalenga kuupunguza: utegemezi mkubwa kwa kampuni kubwa za teknolojia za Marekani. Kampuni za Ujerumani kama Siemens na SAP tayari zinafanya kazi kuhakikisha Ulaya inapunguza utegemezi wake kwa teknolojia ya Marekani, ingawa zinasema kujitenga kabisa si jambo linalowezekana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Digital Industries wa Siemens, Cedrik Neike, aliiambia DW kuwa ni "kosa kubwa kufikiri” Ulaya itaweza kuzalisha kila aina ya programu za Ulaya au kompyuta binafsi zenye GPU na vipengele vyote vinavyohitajika.
"Ukweli ni kwamba dunia imeungana na kutegemeana sana. Tunaweza kupunguza hatari, lakini hatuwezi kamwe kuondoa utegemezi kabisa,” alisema.