1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wenye mzio wadhurika na chanjo ya Pfizer, Uingereza

15 Desemba 2020

Ujerumani Jumatano hii inaanza kufunga shughuli ili kukabiliana na kusambaa zaidi kwa virusi vya corona, huku Uingereza ikiwaonya watu wenye historia ya mzio kupata chanjo ya Pfizer.

UK Coventry | Impfzentrum
Picha: Steve Parsons/AFP

Ujerumani kesho Jumatano inaanza kutekeleza vizuizi vya kufunga shughuli nchini humo ikiwa ni sehemu za harakati zake za kukabiliana na kusambaa zaidi kwa virusi vya corona. Ujerumani inaingia katika hatua hiyo wakati kukiripotiwa kuongezeka kwa visa vipya vya maambukizi. Huku hayo yakiendelea, Uingereza iliyoanza kutoa chanjo wiki iliyopita, imewatahadharisha watu wenye historia ya maradhi ya mzio kutopewa chanjo hizo ya BioNTech/Pfizer baada ya watu wawili waliochanjwa kuugua. 

Idadi ya maambukizi nchini Ujerumani imeongezeka. Kulingana na taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya Robert Koch inayoarifu kuhusiana na maradhi ya COVID 19 nchini Ujerumani, idadi ya maambukizi mapya imeendelea kuwa juu, wakati jana ikiripoti visa vipya 16,362, ikiwa ni ongezeko la visa 4,000 zaidi ikilinganishwa na wiki iliyopita.

Kizuizi cha kufunga shughuli ambacho kilitarajiwa kuondolewa Januari 10 mwakani, huenda sasa kikaendelea kutekelezwa, hii ikiwa ni kulingana na mkuu wa utumishi wa kansela Angela Merkel, Helge Braun, alipozungumza na kituo cha utangazaji cha RTL hapo jana.

Rais wa shirikisho la Ujerumani Frank Walter Steinmeier alipozungumza baada ya vizuizi hivyo kutangazwa na kansela, alitoa mwito kwa umma kushikamana na kuwa na matarajio chanya kufuatia vizuizi hivyo vikali. Amesema, wiki zijazo zitakuwa ni kama majaribio kwa kila mmoja, na kusema ana imani kwamba halitavuruga mustakabali wa ulimwengu na kwamba watalidhibiti janga hilo.

Alisema "Wakati maelfu ya watu wanaambukizwa virusi hatari kila siku na mamia wanakufa. Wakati madaktari na wauguzi wa ICU na nyumba za wazee tayari wamefikia ukomo wao, hii sasa inamaanisha kuwa juhudi zetu za kupambana na janga hili hazitoshi. Tunahitaji kuchukua hatua zaidi. ”

Chanjo ya Pfizer iliyoanza kutolewa kwenye mataifa ya Uingereza na Marekani.Picha: imago images/Political-Moments

Chanzo kimoja ambacho hakikutaja jina lake, kimezungumza na shirika la habari la DPA kuhusiana na suala la chanjo na kusema dozi zinatarajiwa kuhifadhiwa katika kambi iliyoko kwenye mji wa Quakenbrueck kabla ya kusambazwa kote Ujerumani.  Hata hivyo, wizara ya ujenzi ilikataa kuzungumzia chochote taarifa hiyo.

Vyanzo vingine vinasema, mpango huo wa chanjo umeendelea kufanyika kwa siri kwa wiki kadhaa sasa ili kuzuia uingiliaji kutoka kwa wakosoaji, ikiwa ni pamoja na wale wanaotilia shaka chanjo hiyo. Wabunge wa upinzani wanakosoa namna serikali ya Merkel inavyokabiliana na virusi hivyo, lakini pia namna ilivyojiandaa kwa ajili ya chanjo.

Uingereza imeanza kushuhudia changamoto za chanjo.

Wakati haya yakiendelea, huko nchini Uingereza kuna taarifa kwamba watu wawili waliopatiwa chanjo dhidi ya COVID 19, wameugua, hii ikiwa ni pigo kwa mpango huo katika siku zake za mwanzoni. Mwanamke wa kwanza kupata chanjo hiyo baada ya majaribio nchini humo hata hivyo amesema anajisikia vizuri, lakini wasimamizi wa chanjo hiyo wamewatahadharisha watu wenye historia ya maradhi ya mzio kutopewa chanjo hiyo ya Pfizer baada ya watumishi wawili wa afya kuugua baada ya kuchanjwa.

Kwenye taarifa yao, mkurugenzi wa tiba wa shirika la afya la kitaifa, NHS, Steven Powis wamesema ushauri huo unafuatia watu hao wawili wenye historia ya maradhi hayo, kuonesha dalili mbaya na kuugua baada ya kuchanjwa.

Kwingineko, nchini Denmark kumeripotiwa visa vipya 2,558, ikiwa ni idadi mpya ya juu kabisa katika kipindi cha masaa 24. Ni siku ya tatu mfululizo kwa taifa hilo kurekodi visa vipya zaidi ya 2,000 kwa siku.

Nchini Urusi, ambako utoaji mkubwa wa chanjo umeanza mwishoni mwa wiki, kumeripotiwa visa vipya zaidi ya 5,100 na vifo 75.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema COVID 19 huenda yakawa ni maradhi kumi ya mwanzo yaliyosababisha vifo vingi zaidi kwa mwaka 2020, katika wakati ambapo tayari zaidi ya watu milioni 1.5 wakiwa wamefariki kutokana na maradhi hayo hadi sasa.

Mashirika: DPAE