Wenye virusi vya HIV kuishi zaidi
11 Mei 2017Nchini Uingereza wenye virusi na wasio na virusi wanaweza kuishi karibu umri sawa. Unajua kuna ile hali iliyozoeleka ya unyanyapaa na mambo mengine yanayofanana na hayo kuwa ukiwa na virusi vya ukimwi basi wewe upo katika hatihati, sasa wataalamu wanaendelea kuuthibitisha ulimwengu kuwa jambo hilo kwa sasa si sahihi kabisa. Dawa mpya ya maradhi hayo inayoitwa antiretroviral therapy ina uwezo ya kuiongeza umri wa kuishi kwa wenye maradhi kwa takribabni miaka 10. Watafiti wa Uingereza wanasema dawa hizo zimeonesha matumaini katika maeneo ya Ulaya na Marekani. Kwa mujibu wa jarida la masuala ya kisayansi Lancet Medical Journal mafanikio hayo makubwa yanatokana na jitihada za muda mrefu za kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi. Watafiti walifanya utafiti wao katika mataifa 18 ya Ulaya na Amerika ya Kaskazini kwa kujumisha watu 88,504. Kutokana na kuonyesha ishara njema shirika la afya ulimwenguni WHO limependekeza zitolewe kwa umma kadri itakavyowezekana kuweza kunusuru maisha ya wengi. Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa mtu wa umri wa miaka 21 aliyeanza matibabu mwaka 2008 au baadaye anaweza kuishi mpaka kufikia umri wa miaka 70. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni mbili wanaishi na Virusi vya UKIMWI katika mataifa ya Ulaya na huko Amerika Kaskazini.
Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Iddi Sssessanga