Timo Werner ana matumaini ya kukata nyavu tena
5 Machi 2021Chelsea iliipiku Liverpool bao 1-0 katika mechi ya ligi ya Premier iliyochezwa Alhamisi. Bao lilitiwa kimyani na Mason Mount dakika ya 42 ya mchezo na wala sio Timo Werner.
Werner alipachika wavuni mabao matano katika mechi 25 tangu aliposaini mkataba na klabu yake ya zamani ya Bundesliga ya RB Leipzig kwa kitita cha euro milioni 50 msimu uliopita.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alishindwa kucheka na wavu katika mechi 14 mfululizo za ligi kati ya Novemba na Februari kabla kufunga bao katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Newcastle United mwezi huu.
"Ilikuwa ngumu kwangu kwa sababu nilitaka kuisaidia timu," Werner aliiambia BBC. "Nataka kufunga magoli, ni asili yangu, mimi ni mshambuliaji. Sijawahi kukabiliwa na hali hii katika taaluma yangu. Kila mara unajifunza kutokana na hali mbaya. Nimejifunza kujiamini mwenyewe, kufanya bidii kwa nguvu zote uwanjani, sio tu kufikiri kuhusu mabao na kupambana kwa ajili ya timu. Natumai kipindi hiki kimeshapita na nitafunga magoli zaidi mpaka mwisho wa msimu."
Werner alimtaja mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba, aliyevumilia hali ngumu kama yake na kafunga mabao 10 tu katika msimu wake wa kwanza Stamford Bridge baada ya kuwasili akitokea Olympique de Marseille.
Hata hivyo, mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ivory Coast alifanikiwa na kuwa kipenzi cha mashabiki, akiisaidia klabu hiyo ya jiji la London kushinda mataji manne ya ligi ya Premier na kombe la klabu bingwa barani Ulaya mara mbili.
"Washambuliaji wengi wazuri huja kucheza katika ligi ya Premier na huchukua mwaka mmoja kuzowea na kubadili jinsi wanavyocheza," alisema Werner.
"Nadhani hali yangu ya mchezo inapanda na inaboreka zaidi. Pengine mwaka huu si mwaka wa kufunga mabao kwa Timo lakini mwishoni nitafanya tathmini ya msimu."
(reuters)