Westerwelle ataka msimamo wa EU kuhusu Belarus
3 Januari 2011Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle amesema kuwa Umoja wa Ulaya unatakiwa kutoa jibu la wazi la kisiasa juu ya ukandamizaji unaofanywa chini ya utawala wa Rais Alexander Lukashenko nchini Belarus. Matamshi hayo ni kwa mujibu wa gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung.
Westerwelle amesema Umoja wa Ulaya unatakiwa kukabiliana na uongozi wa kisiasa wa Belarus kutokana na taarifa za rushwa katika uchaguzi na ukandamizaji nchini humo.
Ujerumani imekuwa miongoni mwa wakosoaji wakali wa Belarus, wakati ambao nchi hiyo inaendelea kuwashikilia mamia ya wafuasi wa upinzani ambao walikamatwa wakati wa maandamano makubwa kupinga uchaguzi wenye utata wa Desemba 19, uliompa ushindi Lukashenko.
Siku ya Ijumaa, Belarus iliamuru kufungwa kwa ofisi ya Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, kwenye mji mkuu wa Minsk, baada ya shirika hilo kukosoa vikali uchaguzi huo.