Westerwelle aungwa mkono na FDP
31 Agosti 2011Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha SPD Andrea Nahles, amesema, Westerwelle hajidhuru yeye binafsi tu, bali hata chama chake na serikali ya mseto ya Ujerumani. Ameliambia gazeti la Morgen Post, sera za waziri wa nje Guido Westerwelle, zinachafua taswira ya Ujerumani. Mwanasiasa huyo wa SPD akiwakosoa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wa chama cha CDU na makamu wake Philipp Roesler wa FDP, alisema wakimuachia Westerwelle kuendelea kuvuruga mambo, basi wanasiasa hao wanayatanguliza maslahi yao binafsi na sio ya taifa la Ujerumani.
Hapo jana, Phillip Roesler,alie pia mwenyekiti wa FDP, alisema mdahalo kuhusu kujiuzulu kwa Westerwelle umemalizika. Viongozi wa chama hicho wanamuunga mkono waziri wa mambo ya nje wa hivi sasa Westerwelle. Na hata katika siku zijazo hilo halitobadilika alisisitiza Roesler alipozungumza kwenye mkutano wa viongozi na wabunge wa FDP huko Bergisch Gladbach.
Hata Katibu Mkuu wa chama cha FDP, Christian Lindner akijaribu kuumaliza mdahalo huo, alisema, Westerwelle ametekeleza miradi muhimu na anaungwa mkono kwa hayo yote, alisisitiza Lindner. Amesema,mdahalo huo kuhusu Westerwelle, kwa sehemu kubwa unachochewa na wanasiasa wa upinzani. Uvumi kuwa Westerwelle atatimuliwa ikiwa chama cha FDP kitashindwa katika chaguzi mbili zijazo majimboni, ni dhana zisizo na msingi.
Kwa upande mwingine, mwenyekiti wa chama cha SPD, Sigmar Gabriel amemtaka Kansela Merkel kuchukua hatua. Amesema,Kansela hawezi kuiachilia Ujerumani kupoteza uaminifu wake katika nchi za nje. Akasisitiza kuwa Kansela anawajibika kwa makosa yote yaliyofanywa na waziri wa nje Westerwelle. Amesema, sasa ni lazima kwa serikali kuwa tena na sera za nje zinazoaminika.
Waziri Westerwelle alianza kulaumiwa vikali, alipozuia kura ya Ujerumani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuunga mkono operesheni ya jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Libya mnamo mwezi wa Machi mwaka huu. Na hivi karibuni badala ya kuisifu waziwazi operesheni ya NATO alisema, sera ya kuiwekea vikwazo Libya ndiyo iliyosaidia kuuangusha utawala wa Muammar Gaddafi. Baadaye alikiri hadharani kuwa Walibya ndio walioipindua serikali ya Gaddafi kwa msaada wa NATO.
Kwa maoni ya viongozi na wabunge wa FDP wanaokutana Bergisch Gladbach mdahalo wa Westerwelle umemalizika. Mkutano wao sasa unashughulikia mpango wa kuiokoa sarafu ya Euro, sera za kiuchumi katika masoko ya dunia, haki za raia, na elimu.
Mwandishi: Martin, Prema/dpa
Mhariri: Josephat Charo