WFP: Sudan hatarini kukumbwa na baa kubwa la njaa
15 Desemba 2023Katika taarifa yake, WFP imesema kuwa baadhi ya sehemu zilizokumbwa na vita nchini Sudan zinakabiliwa na hatari kubwa ya kutumbukia katika hali mbaya ya janga la njaa kufikia msimu ujao wa kiangazi.
Shirika hilo limesema kuwa hali hii inaweza ikifanya wakashindwa kufikia na kuongeza msaada wa mara kwa mara wa chakula kwa watu waliokwama katika maeneo ya vita ukiwemo mji mkuu Khartoum.
Soma zaidi: WFP: Njaa kali itaongezeka nchini Somalia kufuatia mafuriko
Siku ya Jumatano WFPilisema kuwa takribani watu milioni 18 nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali, hii ikiwa ni mara mbili zaidi ya idadi sawa ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita.
Taarifa ya WFP imeendelea kusema, utafiti mpya wa hali ya chakula nchini Sudan, unaonesha viwango vya juu zaidi vya njaa kuwahi kurekodiwa wakati wa msimu wa mavuno ambao ni mwezi Oktoba hadi Februari, ambapo kwa kawaida chakula zaidi hupatikana.
Siku ya Jumapili, Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja huo nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa, WFP imeweza kufikia sehemu ndogo tu ya watu karibu milioni 25 wanaohitaji msaada.
Nkweta-Salami, ameongeza kuwa hata msaada kwa watu milioni 4 wanaoweza kufikiwa huenda ukakatizwa karibuni iwapo ukosefu wa ufadhili utakithiri.
Mzozo wa kivita umetajwa kuchangia ongezeko la baa la njaa
Mkurugenzi na muwakilishi wa WFP nchiniSudan, Eddie Rowe alisema kuwa shirika hilo linazitaka pande mbili zenye mzozo nchini humo kusitisha mapigano kuwezesha kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu ili kuepusha janga la njaa.
Hata hivyo, kuzileta pamoja pande zinazozozana kwa mazungumzo bado ni suala gumu huku pande zote mbili zikilaumiwa kwa kuvunja makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano.
Kwa mujibu wa shirika linaloangazia maeneo yenye mizozo ya vita na takwimu la Armed Conflict Location & Event Data Project, miaka miwili baada ya washirika hao wa zamani kupanga na kufanya kwa pamoja mapinduzi ya mwaka 2021 dhidi ya serikali ya Bashir, ambayo ilivuruga mageuzi dhaifu ya kidemokrasia, mzozo wao wa kuwania madaraka umesababisha vifo vya zaidi ya watu 12,190.
Umoja wa Mataifa umerekodi watu milioni saba waliokimbia makazi yao kote Sudan, ikijumuisha na ukosefu wa mavuno mazuri, hukui baa la njaa inashuhudiwa katika sehemu kubwa ya nchi hiyo.
Maeneo yaliyo hatarini zaidi ni Darfur Magharibi na Kordofan Kusini, pamoja na mji mkuu Khartoum, ambako mzozo huo ulizuka mara ya kwanza.