1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

WFP: Watoto laki 6 wakosa msaada Sudan Kusini

Dotto Bulendu
9 Mei 2025

Umoja wa Mataifa umesema mapigano ya Sudan Kusini yanayoendelea yanazuia juhudi za kufikisha misaada kwa watoto wapatao 60,000 wanaokabiliwa na utapiamlo kutokana na ukosefu mkubwa wa chakula.

Hali kwenye mpaka wa Sudan Kusini na Sudan
Mapigano nchini Sudan Kusini na wimbi la wakimbizi kutoka taifa jirani la Sudan vyote vimezidisha wasiwasi wa kukosekana chakula na waathiriwa wakubwa ni watoto.Picha: Sally Hayden/SOPA Images/ZUMA Press Wire/picture alliance

Kwa mujibu wa Shirika la Misaada ya Chakula la Umoja wa mataifa (WFP) na lile wa Watoto (UNICEF), hali katika jimbo la Upper Nile imezidi kuwa mbaya.

Mashirika hayo yameelezea wasiwasi wao kuhusu kukwama shughuli zake za usambazaji wa lishe katika jimbo hilo, ambalo lina viwango vya juu zaidi vya utapiamlo nchini Sudan Kusini iwapo hali haitabadilika kufikia mwishoni mwa mwezi huu. Mwakilishi wa UNICEF Obia Ochieng, amesema katikati ya mwezi Aprili, majahazi yaliyobeba tani takriban elfu moja za chakula na vifaa vya lishe kuelekea jimbo hilo la Upper Nile yalishindwa kufikisha bidhaa hizo kutokana na ukosefu wa usalama katika eneo linalokabiliwa na mapigano la Kaskazini mwa Sudan ya Kusini.Eneo la kaskazini mwa nchi hiyo tayari lina zaidi ya watoto 300,000 wanaoathiriwa na utapiamlo tangu mwaka uliopita na hali inazidi kuwa mbaya.

Ochieng amesema uamuzi wa kusitisha zoezi la kusafirisha vyakula ulitokana na hofu ya kutowafikia walengwa kutokana na mapigano yanayoendelea pamoja na uporaji na usumbufu katika njia ya mtoni.

Mashirika: Watoto wadogo ndio wapo hatarini zaidi

Mashirika yote mawili ya Umoja wa Mataifa yametahadharisha juu ya kuyumba kwa hali ya usalama nchini Sudan Kusini ambayo inaleta hofu ya maafisa wake kuwa walengwa wa mashambulizi ya kundi la wanamgambo wa kabila la Nuer.

Ukosefu wa chakula ni tishio kwa maisha ya watu nchini Sudan Kusini. Picha: DW

Yamesema iwapo hali hii itaendelea, basi kaunti kadhaa katika jimbo lote la Upper Nile litakumbwa na hatari ya kukosa mahitaji na vifaa kufikia mwisho wa mwezi na matokeo mabaya yatakuwa hasa watoto wadogo, ambao ndio wako hatarini zaidi.

Taifa changa la Sudan Kusini limekumbwa na hali ya ukosefu wa usalama na ukosefu wa utulivu wa kisiasa kwa miaka mingi, lakini mapigano ya hivi majuzi katika Jimbo la Upper Nile kati ya vikosi vinavyomuunga mkono Rais Salva Kiir na mpinzani wake, Makamu wa Rais wa kwanza Riek Machar, yamewatia wasiwasi wadau wanaofuatilia matukio ya nchini humo.

Mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Sudan Kusini umesababisha kukamatwa kwa Makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa mzozo huu unaweza kuzusha vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo baada ya kumalizika mgogoro wa mwaka 2018.