1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WFP: Watu milioni 24 duniani wataingia kwenye baa la njaa

14 Septemba 2023

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limetahadharisha watu zaidi ya milioni 24 wanakabiliwa na hatari ya kutumbukia kwenye baa la njaa ulimwenguni ikiwa hatua za haraka hazitochukuliwa.

Naibu wa shirika la Mpango wa chakula Umoja wa mataifa WFP Ute Klamert
Naibu wa shirika la Mpango wa chakula Umoja wa mataifa WFP Ute KlamertPicha: WFP/Rein Skullerud

Shirika hilo la mpango wa chakula duniani limethadharisha kwamba kupungua kwa fedha za msaada kunailazimisha taasisi hiyo kupunguza kwa kiwango kikubwa mgao wake  katika operesheni zake nyingi kwenye maeneo yalioathirika.

Kimsingi shughuli za shirika hilo ni pamoja na miradi ya kugawa chakula cha msaada lakini limekuwa likihangaika kutafuta suluhisho la mahitaji yanayoongezeka duniani ya kutowa msaada wa chakula.

Soma pia:WFP: Njaa itaongezeka baada ya ufadhili kupungua

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linakabiliwa na upungufu wa fedha wa zaidi ya asilimia 60 kwa mwaka huu.

Upungufu huo wa fedha ndio mkubwa zaidi kuwahi kulikumba shirika hilo tangu kuanzishwa kwake.

Kupitia taarifa iliyotolewa na shirika hilo, inaonesha kwa mara ya kwanza kabisa WFP linashuhudia upungufu mkubwa wa msaada wa wafadhili huku kwa upande mwingine mahitaji yakiongezeka kwa kiwango kikubwa. 

Wataalamu wafafanua ukubwa wa tatizo

Wataalamu katika shirika hilo wanatahadharisha kwamba hatua hii inaweza kuwa na athari mbaya huku wakitowa makadirio yanayoonesha kwamba kwa kila pacenti moja ya kupunguzwa kwa msaada wa chakula,zaidi ya watu 400,000 wanaingia  katika hatari ya kutumbukia katika viwango vikubwa vya njaa.

Maafisa wa WFP wakiandikisha wasudani wanaotarajiwa kupata masaada wa chakulaPicha: Mahamat Ramadane/REUTERS

Kutokana na kupunguzwa kwa fedha za msaada shirika la WFP limesema linalazimika kutahadharisha kwamba idadi ya watu milioni 24 zaidi huenda wakatumbukia kwenye baa la njaa katika kipindi cha zaidi ya miezi 12 ijayo.

Hiyo ikiwa ni ongezeko la  asilimia 50 ya kiwango cha idadi ya sasa ya walioko hatarini.

Mkuu wa shirika la WFP Cindy McCain amesema fedha zaidi zinahitajika ili kuepusha janga zaidi.

Soma pia:WFP kupunguza misaada ya chakula kwa mamilioni ya watu wa Afghanistan

Amebaini kwamba ikiwa fedha hazitopatikana   kuepusha janga hilo hapana shaka ulimwengu utashuhudia migogoro zaidi,machafuko na njaa zaidi.

Mkuu huyo wa WFP kwahivyo ametowa mwito kwamba ni ama ulimwengu ushirikiane kuuchochea ukosefu wa uthabiti au ufanye kazi kwa mshikamano na kwa haraka kuuzima moto. 

Shirika hilo linakadiria kwamba watu milioni 345 duniani wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula,uliofikia kiwango cha tatu au hata zaidi katika kipimo cha tano cha viwango vya ukosefu wa usalama wa chakula vinavyofahamika kama IPC. 

Watu mil. 40 wataingia katika hali ya dharura

Kufikia sasa idadi ya watu milioni 40 wanatazamwa kuwa katika viwango vya dharura vya ukosefu wa chakula,ikimaanisha kwamba ni watu wanaolazimika kuhangaika  kutafuta namna ya kuokoa maisha yao kwa hali yoyote na wako kwenye hatari ya kupoteza uhai kutokana na utapiamlo.

Magari ya WFP yakifikisha msaada wa chakula SudanPicha: Mahamat Ramadane/Reuters

Mara nyingi shirika la WFP ndio mahala pekee wanakotegemea kuepuka baa la njaa kwa kupokea msaada muhimu wa kuyaokoa maisha yao.

Kwa bahati mbaya shirika hilo sasa linasema linalazimika kupunguza kwa takriban nusu ya shughuli zake  ikiwemo katika maeneo tete kama Afghanistan,Bangladesh,Haiti na Syria.

Nchini Afghanistan kwa mfano ambako nusu ya idadi ya watu wake wanakabiliwa na ukosefu mkubwa sana wa usalama wa  chakula ,WFP lililazimika mwezi Mei kupunguza shughuli zake kwa asilimia 66. 

Soma pia:Shirika la WFP larejesha msaada wa chakula Ethiopia

Hatua hiyo inamaanisha kwamba kiasi watu milioni 8 wanaohitaji msaada hawawezi kupokea tena msaada huo wa chakula.Na katika mwezi wa Julai asilimia 45 ya wanaopokea msaada nchini Syria na robo ya wale waliokuwa kwenye orodha ya WFP nchini Haiti walikatiwa misaada.

Halikadhalika shirika hilo limesema limelazimika pia kupunguza takriban nusu ya operesheni zake nchini Somalia hatua iliyowaathiri watu milioni 4.7,wakati nchi hiyo ikiwa inashuhudia kilele cha ukame mwishoni mwa mwaka jana.

Na hivi sasa wataalamu hao wa chakula wa Umoja wa Mataifa wanakhofia kwamba janga kubwa la kibinadamu linafukuta na linatowa raia kwa wafadhili na ulimwengu kwa ujumla wake kuwaokoa wanaokabiliwa na njaa na njia pekee ni kutolewa ufadhili wa operesheni za misaada ya dharura.

Kilio cha njaa, Somalia

02:29

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW