1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Njaa yawanyemelea watu wa Cabo delgado nchini Msumbiji

7 Julai 2021

Hali ya maisha ya watu wa Cabo Delgado inategemea msaada wa WFP na washirika wake

Mosambik I Nahrungsmittelknappheit in Cabo Delgado
Picha: Falume Bachir/World Food Program/AP/picture-alliance

Zaidi ya watu 730,000 wameachwa bila makaazi huko kaskazini mwa Mumbiji kutokana na mgogoro uliolikumba eneo hilo. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula linasema eneo hilo linaweza kukabiliwa na njaa ikiwa msaada wa haraka wa fedha hautopatikana.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, lilitowa tahadhari jana Jumanne kwamba watu wa kaskazini mwa Msumbiji wanahitaji msaada wa haraka wa fedha, dola milioni 121 kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika kutokana na mgogoro huko Kaskazini mwa Msumbiji. Shirika hilo linasema fedha hizo zitawasaidia watu wa eneo hilo hadi mwishoni mwa mwaka huu lakini likatahadharisha kwamba hueka likajikuta kulazimika kuanza kupima mgao au kusisitisha kabisa utoaji wa chakula mwezi Agosti ikiwa fedha hazitopatikana.

Picha: Falume Bachir/World Food Program/AP/picture-alliance

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeweka wazi kwamba watu zaidi ya 730,000 walioachwa bila makaazi kaskazini mwa Msumbiji huenda wakakabiliwa na hali ya dharura ya njaa ikiwa fedha zilizotajwa hazitopatikana haraka. Mkurugenzi mtendaji wa WFP David Beasley akizungumzia hali ya Msumbiji amesema shirika hilo linawahudumia watu 715,000 kwa sasa kaskazini mwa nchi hiyo.

"Hili lilikuwa eneo la kitalii, uvuvi, uchumi ulikuwa mzuri watu walikuwa na maisha mazuri, lakini unajua nini kilichofanyika? Wanamgambo, magaidi walikuja na kuzitenganisha familia, kuchoma makaazi yao, kuua watu, kubaka wanawake, na kuharibu kabisa maisha ya watu na kwa hivyo WFP iko hapa sasa hivi kujaribu kuwapa matumaini watu. Watu 715,000 tunaowasaidia hivi sasa.''

Wanamgambo wa jihadi wamekuwa wakiendesha vurugu katika mkoa wa Cabo Delgado tangu mwaka 2017 ambapo mashambulizi yao yaliongezeka mwaka jana. Mkoa huo wenye utajiri wa gesi umeharibiwa kabisa tangu wanamgambo hao wanaofungamanisha na kundi la kigaidi linalojiita dola la kiislamu kufanya uvamizi wa ghafla mnamo mwezi March na kuua watu chungunzima na kuwalazimisha maelfu kukimbia.

Picha: Falume Bachir/World Food Program/AP/picture-alliance

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, David Beasley amesena watu wasiokuwa na hatia wa jamii hii ya wanamsumbiji hivi sasa wanalitegemea shirika hilo na washirika wake kwa kila kitu ikiwemo chakula kunusuru maisha yao.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW