WFP yasema bado msaada kwa Gaza ni mdogo
17 Oktoba 2025
Msemaji wa shirika hilo la WFP Abeer Etefa, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba bado kiwango cha msaada kiko chini ya kile kinachohitajika lakini wanaendelea kupiga hatua.
Etefa amesema usitishwaji wa mapigano umefungua fursa ndogo ya kuingiza msaada na WFP inasonga mbele kwa haraka kuongeza msaada wa chakula na kufikia familia ambazo zimevumilia miezi ya kufungwa kwa vivukio, kupoteza makazi na baa la njaa.
Hata hivyo WFP imesema bado haijaanza usambazaji katika mji wa Gaza City, na kusema hilo limesababishwa na kuendelea kufungwa kwa vivuko viwili vya mpaka, Zikim na Erez, huku Israel ikidhibiti kaskazini mwa eneo hilo ambako mzozo wa kibinadamu ni mkubwa zaidi.
Misafara ya misaada bado inashindwa kusambaza msaada Gaza
Ingawa kiwango kidogo cha bidhaa za lishe bora kimefika kaskazini, misafara ya misaada bado haiwezi kupeleka kiwango kikubwa cha chakula katika eneo hilo, pamoja na maeneo mengine.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kiutu, OCHA, imesema malori 950 yaliingia Gaza jana Alhamisi ikijumuisha kutoka sekta ya biashara, michango ya nchi na mfumo unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa, kupitia vivuko vya Kerem Shalom na Kissufim, ikinukuu takwimu za mamlaka ya Israel inayosimamia masuala ya kiraia katika maeneo ya Palestina COGAT, zilizowasilishwa kwa wapatanishi.
Hamas yataka hatua zaidi ya makubaliano kutekelezwa
Huku hayo yaijiri, Kundi la Hamas, leo limetoa wito kwa wapatanishi katika mzozo wake na Israel, kushinikiza kuchukuliwa kwa hatua zinazofuata chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ikiwa ni pamoja na kufungua mipaka, kuingizwa kwa misaada, kuanza ujenzi mpya, kuanzisha utawala na kukamilisha kuondoka kwa vikosi vya Israel Gaza.
Wataalamu wa Uturuki wasubiri idhini ya Israel kuingia Gaza
Makumi ya wataalamu wa Uturuki waliotumwa na nchi yao kusaidia kutafuta miili katika ukanda wa Gaza kwa sasa wako kwenye mpaka wa Misri, wakisubiri idhini kutoka kwa serikali ya Israeli. Haya ni kwa mujibu wa afisa mmoja wa Uturuki aliyeliarifu shirika la habari la AFP.
Afisa huyo amesema timu ya maafisa 81 wa taasisi ya shughuli za utafutaji na uokoaji wanasubiri mpakani katika upande wa Misri lakini haijabainika wazi ikiwa Israel itairuhusu timu hiyo kuingia Gaza.