WFP: Wayemen milioni 13 huenda wakakabiliwa na njaa
24 Februari 2022Katika mahojiano yake na shirika la habari la AP Alhamisi, David Beasley amesema Yemen iko katika hali mbaya, huku zaidi ya asilimia 40 ya watu wake wakiwa tayari wanategemea msaada wa chakula kutoka WFP.
Akizungumza kutoka kwenye mji mkuu wa Yemen, Sanaa Beasley amesema shirika hilo linatoa chakula kwa watu milioni 13 kati ya watu milioni 30 wa Yemen na wanakabiliwa na uhaba wa pesa.
COVID-19 yasababisha watu zaidi kukabiliwa na njaa
Amesema tangu kuzuka kwa janga la COVID-19, watu wengi zaidi wamekuwa wakikabiliwa na kitisho cha njaa ulimwenguni ambacho kimeweka shinikizo kubwa kwa WFP.
Kwa mujibu wa shirika hilo, hivi sasa watu milioni 285 kote ulimwenguni wanakabiliwa na kitisho cha njaa, hali inayofanya kuwa ngumu zaidi kushughulikia mahitaji ya watu wa Yemen.
Beasley amefafanua kuwa wamepata mara mbili idadi ya watu wanaohangaika duniani kwa sasa na hivyo shirika hilo linajiuliza litafanya nini kwa watoto wa Yemen. Anauliza iwapo waibe chakula kutoka kwa watoto wa Ethiopia, au Afghanistan, au Nigeria, au Syria? Anasema kufanya hivyo sio sawa.
Mkurugenzi huyo wa WFP anasema shirika hilo limelazimika kupunguza mgao wake kwa nusu kwa ajili ya watu milioni nane wa Yemen kutokana na uhaba wa fedha. Amebainisha kuwa huenda wakapunguza mgao wote, lakini iwapo hilo litafanyika, watu watakufa na litakuwa janga.
Kwa mujibu wa WFP, takribani watu milioni 811 hawana chakula cha kutosha ulimwenguni kote na linakadiria kuwa watu milioni 45 kwenye nchi 43 wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa.
WFP inahitaji bilioni 9 zaidi
Beasley amesema WFP inahitaji dola bilioni tisa za ziadi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya msaada wa chakula duniani kote. Amedai kuwa kutokana na utajiri wa dola trilioni 430 duniani hii leo, hakuna mtoto hata mmoja anayepaswa kufa kwa njaa kokote kule ulimwenguni.
Licha ya mashambulizi ya anga yasiyomalizika na mapigano ya ardhini, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen vilivyoanza mwaka 2014, vimesababisha mzozo wa kibinaadamu. Tangu wakati huo, Marekani imesitisha ushiriki wake wa moja kwa moja katika mzozo huo.
Beasley anasema nchini Yemen watoto pamoja na familia zao wamelipia gharama ya kutosha kutokana na vita vinavyowakabili na kwamba ni muda sasa wa vita hivyo kumalizika. Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo wa WFP, anachokiona sasa ni watoto na familia zao ambao wanaomba chakula.
(AP)