1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Msaada wa chakula wasitishwa kwa malaki Ethiopia

22 Aprili 2025

Shirika la Mpango wa Chakula Ulimwenguni, WFP limesema linasitisha msaada wa matibabu kwa wanawake na watoto 650,000 wenye utapiamlo nchini Ethiopia kutokana na uhaba mkubwa wa fedha.

Ukame nchini Ethiopia watishia maisha ya watu
Ukosefu mkubwa wa chakula unaotokana na ukame unatishia maisha ya mamia kwa maelfu ya watu nchini Ethiopia. Picha: Mariel Mueller/ Haileselassie Million/DW

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa shirika hilo nchini Ethiopia, Zlatan Milisic imeeleza kuwa watu milioni 10 wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula  na utapiamlo miongoni mwao wakiwa ni wakimbizi wa ndani milioni 3 walioyakimbia makazi yao kutokana na vita na hali mbaya ya maisha hasa kwa wakimbizi wa ndani na wale kutoka nchi jirani ya Sudan wanaokimbia vita na machafuko.

Kupungua kwa misaada ya kifedha kulikotangazwa na WFP kumetokana na nchi wahisani kushindwa kutimiza ahadi zake za michango ya kifedha katika shirika hilo.

Kwa kawaida shirika hilo hupata misaada ya kifedha kutoka nchi wahisani kati ya 15 na 20 ikiwemo Marekani. Nchi hizo zote zikiwemo zile za Magharibi zimepunguza kwa kiasi kikubwa misaada yake kwa shirika hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Uingereza Reuters, hata hivyo utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani haujasitisha misaada ya fedha kwa WFP kama ambavyo Marekani imefanya kwa mashirika mengine, lakini pia huenda lisisaidie lolote katika mwaka huu wa 2025.

Milisic ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba kuanzia sasa hadi mwezi wa tisa shirika hilo linahitaji angalau dola za Marekani milioni 222 ambazo kama hazipatikani maisha ya watu walioathirika kwa vita, ukame na mabaa ya njaa yatakuwa katika hatari.

WFP yaukumbusha ulimwengu hali nchini Ethiopia siyo nzuri 

WFP imetoa mwito kwa ulimwengu na wahisani kutoa fedha kuwasaidia watu wa Ethiopia. Picha: Million Haileselassie Brhane/DW

Aidha, amesema huu ni muda muafaka wa kuukumbusha ulimwengu na wahisani wao kwamba hali ya kibinadamu nchini Ethiopia siyo nzuri na kusema itaendelea kuwa mbaya zaidi.

Amesema awali WFP ilikuwa imepunguza kiasi cha milo kwa waathirika kwa miezi ya hivi karibuni, lakini akaonya kwamba sasa hivi hali imefikia pabaya kutokana na kukosa ufadhili na hivyo kusababisha kuchukuliwa hatua ngumu zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia mtandao akiwa mjini Addis Ababaz, Ethiopia Milisic ameonya kutokea kwa janga zaidi.

Majimbo yatakayoathirika kwa kiasi kikubwa na uamuzi huu wa WFP ni pamoja na Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia ambalo limeharibiwa kwa vita vya wenyewe kwa wenye tangu mwaka 2020 pamoja na majimbo ya Oromia na Amhara ambayo hadi sasa yanakabiliwa na mapigano ya ndani.

Pia kuwepo kwa idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi jirani za Sudan na Somalia kunaliweka shirika la WFP katika wakati mgumu na mahitaji makubwa ya kuwahudumia wakimbizi wenye shida ya chakula na matibabu.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi