1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Chanjo za majaribio za Ebola kupelekwa Uganda

19 Oktoba 2022

Muakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO nchini Uganda Dkt Yonas Tegegn Woldemariam, amesema kuwa chanjo za majaribio za ugonjwa wa Ebola zitapelekwa nchini Uganda katika muda wa wiki mbili zijazo

Uganda Ausbruch von Ebola
Picha: Hajarah Nalwadda/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Dkt Woldemariam, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba maelfu ya dozi hizo za majaribio za chanjo zitaimarisha juhudi za kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huo wa Ebola ambazo bado zitahitajika kulenga kufuatilia waliotangamana na waathiriwa na ushirikiano wa kijamii.

Muakilishi huyo wa shirika la afya ulimwenguni, WHO nchini Uganda amesema huo ni utafiti na mbinu nyingine watakayojaribu. Amesema kuwa chanjo zilizotengenezwa na Taasisi ya Chanjo ya  Sabin yenye makao yake makuu nchini Marekani na Chuo Kikuu cha Oxford, ziko tayari kusafirishwa kuelekea Uganda, ambayo inakamilisha itifaki za utafiti huo kabla ya Mamlaka ya Kitaifa ya Dawa kutoa vibali vya kuziagiza.

Takwimu za Ebola Uganda

Ebola, inayojidhihirisha kama homa inayoambatana na kuvuja kwa damu, imeambukiza watu wasiopungua 60 na kuua 24 nchini Uganda. Takwimu hizo rasmi hazijumuishi watu ambao kuna uwezekano walikufa kutokana na ugonjwa huo wa Ebola kabla ya mlipuko huo kuthibitishwa. Waathiriwa ni pamoja na wafanyikazi watano wa sekta ya afya.

Afisa wa matibabu apuliza dawa katika kituo cha kushughulikia Ebola wilayani Mubende, UgandaPicha: Nicholas Kajoba/Xinhua News Agency/picture alliance

Kulingana na Dkt Yonas Woldemariam ambaye anafuatilia kwa karibu jinsi Uganda inayoshughulikia mlipuko huo, chanjo ya Oxford inatolewa na Taasisi ya Serum ya India, ambayo imeonyesha kuwa hatimaye inaweza kutengeneza maelfu ya dozi.

Uganda ilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mnamo Septemba 20, siku kadhaa baada ya ugonjwa huo wa kuambukiza kuanza kuenea katika jamii ya wakulima ya mashambani.

Hatua za vizuizi na marufuku ya kutotoka nje wakati wa usiku tayari zimewekwa katika kitovu cha mlipuko huo umbali wa kilomita 150 Magharibi mwa mji mkuu wa Kampala.

Ebola huambukizwaje?

Ebola huambukizwa kwa kugusana na maji maji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa ama vifaa vilivyoambukizwa. Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa, kutapika, kuharisha, maumivu makali ya misuli na wakati mwingine kuvuja damu nje na ndani ya mwili. Wanasayansi hawafahamu hifadhi asili ya kirusi hicho, lakini wanashuku kuwa mwathiriwa wa kwanza katika mlipuko wa ugonjwa huo huambukizwa kupitia kugusana na mnyama aliyeuguwa ama kula nyama yake mbichi.

Mafisa nchini Uganda wachunguza chanzo cha mlipuko 

Maafisa nchini Uganda bado wanachunguza chanzo cha mlipuko wa sasa. Uganda imekuwa na mlipuko wa Ebola mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na mwaka wa 2000 ambapo zaidi ya watu 200 walifariki. Mlipuko wa Ebola wa kati ya mwaka 2014 na 2016 huko Afrika Magharibi ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 11,000, hii ikiwa idadi kubwa zaidi kutokana na maambukizo ya ugonjwa huo kuwahi kutokea.