Dunia imeingia hali ya mashaka kufuatia virusi vya Corona
3 Machi 2020Hali ya wasiwasi imetanda barani Ulaya baada ya kurekodi visa vipya vya maambukizi ya Corona, ikiwa ni mara tisa zaidi ya China ambako ni kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.
Kwa mujibu wa shirika la WHO, virusi hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,100 huku watu zaidi ya elfu 90 wakiambukizwa kote duniani.
Kupungua kwa maambukizi mapya nchini China kumehusishwa na mikakati iliyowekwa na mamlaka nchini humo kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo ikiwemo kuzuia mikusanyiko ya watu na kuweka marufuku ya usafiri.
Peng Xiaoxiang ambaye ni mkurugenzi wa hospitali ya muda ya Gymnasium amesema. "Tulitakiwa kujiandaa kwa mlipuko wa Corona lakini sasa tumesimamisha kwa muda oparesheni katika hospitali hii kwa sababu idadi ya wagonjwa imepungua. Hatutaifunga lakini iwapo huduma zetu zitahitajika, basi tuko tayari."
Wakati maambukizi mapya yanapungua China, hali ni tofauti nchini Marekani kwani taifa hilo sasa linakabiliwa na janga kubwa la kusambaa kwa virusi hivyo. Tayari watu sita wamefariki dunia katika jimbo la Washington.
Makamu wa Rais wa Marekani amesema yako matumaini kuwa tiba dhidi ya Corona huenda ikapatikana hivi karibuni
Akizungumzia mlipuko wa virusi vya Corona, Makamu wa Rais Mike Pence amesema yako matumaini kuwa huenda tiba dhidi ya virusi hivyo ikapatikana hivi karibuni.
China imechukua hatua kali za kuweka karantini na kuzuwia usafiri kuzuwia kusaamba kwa virusi hiyo, hatua ambayo inaonekana kuzaa matunda.
Wakati Italia imezuwia miji mizima, mataifa mengine yamejizuwia kuwaweka karantini watu wengi nabadala yake yamejaribu kuzuwia mikusanyiko mikubwa, kuchelewesha matukio ya kimichezo na kupiga marfuku abiria kutoka mataifa yalioathirika zaidi.
Korea Kusini, Iran na Italia ni mataifa ya karibuni ambayo yamekumbwa na mlipuko wa virusi vya Corona, vinavyoaminika kuanzia katika soko linalouza wanyama pori kama kitoweo katika mji wa Wuhan mwishoni mwa mwaka uliopita.
Kutokana na wasiwasi juu za athari za virusi hivyo kwa uchumi wa dunia, mawaziri wa fedha wa nchi zenye nguvu kubwa kiuchumi duniani G7, pamoja na magavana wa benki kuu za mataifa hayo watafanya mkutano kuhusu suala hilo leo Jumanne.
Wakati huo huo, gazeti moja la Italia limeripoti kuwa Papa Francis ambaye amekuwa akisumbuliwa na homa, amepimwa na kugunduliwa kuwa hana virusi hivyo.
Hofu iliibuka kuwa huenda kiongozi huyo wa kidini mwenye miaka 83 ameambukizwa virusi vya Corona baada ya kuonekana akikohoa na kupiga chafya japo Vatican ilikanusha uvumi kuwa Papa Francis alikuwa ameambukizwa virusi vya Corona.
Vyanzo AFP/DPA