1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Hatua nzuri katika kupambana na magonjwa ya kitropiki

Daniel Gakuba
19 Aprili 2017

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limesema hatua imepigwa katika kupambana na magonjwa ya Ukanda wa Tropiki, na kuyahimiza makampuni ya kutengeneza dawa kuongeza ufadhili katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Gabun Albert-Schweitzer Klinik Ärztin untersucht Blutproben
Utafiti umepiga hatua katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kitropikiPicha: DW/G. Manco

Ripoti hiyo inayahusu magonjwa 18 yanayotibika kirahisi, ambayo lakini yamekuwa yakiwasumbua watu takribani bilioni moja wa nchi za ukanda wa Tropiki katika mabara ya Afrika, Asia na Amerika Kusini. Magonjwa hayo yanafahamika kama 'maradhi yaliyosahaulika' kwa sababu hayapewi umuhimu mkubwa na makampuni ya utafiti, kwa vile hayapo katika nchi tajiri duniani.

Magonjwa hayo ambayo ni pamoja na homa ya denge, usubi (river Blindness) na malale, ni miongoni mwa yale yanayoambukizwa na mbu na inzi, na yamekuwa yakienea kutoka vijijini hadi mitaa ya mabanda katika maeneo ya miji.

Akizungumza na waandishi wa habari, mkurugenzi anayehusika na magonjwa yaliyosahaulika katika shirika la afya ulimwenguni, Dkt Dirk Engels, amesema hakuna magonjwa ambayo yanahusiana zaidi na umasikini kuliko hayo ya ukanda wa Tropiki. Imeelezwa kuwa magonjwa hayo huuwa watu zaidi ya 170,000 kila mwaka na kuwaacha wengine na ulemavu wa kudumu.

Kutokana na juhudi za matibabu, idadi ya wanaoathiriwa na magonjwa hayo imeshuka kutoka watu bilioni mbili mwaka 2010 hadi bilioni 1.6 mwaka huu. Karibu theluthi moja ya walioathiriwa ni watoto wadogo.

Bado njia ni ndefu

Dkt Engels amesema wanashirikiana na makampuni kadhaa maarufu ya kutengeneza dawa, kama vile GlaxoSmithKline, Novartis na Sanofi, na kuongoza lakini kuwa hatua iliyopigwa haitoshi, kwa sababu bado upo ukosefu wa dawa, na magonjwa hayo hayajapewa kipaumbele kama inavyostahili.

Mgonjwa wa usubi, ugonjwa unaosababisha upofuPicha: AFP/Getty Images

Mkurugenzi mkuu wa WHO Margaret Chan amesifu ushirikiano unaoongozwa na wakfu wa bilionea wa Kimarekani Bill Gates na mkewe Belinda, katika kuwanusuru mamilioni ya watu kutokana na magonjwa hayo ambayo huandamana na ulemavu na umasikini.

Bill Gates amesema yapo matumaini ya kuyatokomeza kabisa baadhi ya magonjwa hayo ifikapo mwaka 2020, na mengine kuondolewa kabisa miaka mitano baadaye.

Juhudi za pamoja zazaa matunda

Shirikisho la makampuni ya watengenezaji wa dawa, IFPMA limesema hivi sasa upo utafiti wa aina 109 unaoendelea, kutengeneza dawa na kinga dhidi ya magonjwa hayo yanayopuuzwa, utafiti ambao kwa wasitani huchukua muda wa miaka kati ya 10 na 15.

Bila kuushinda umasikini, juhudi dhid ya magonjwa hayo zitakwama-WHOPicha: AP

Juhudi dhidi ya magonjwa hayo ya kitropiki yaliyosahaulika zilishika kasi mwaka 2012 baada ya makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa mjini London kati ya serikali za mataifa na makampuni ya dawa, wakiahidi kuchangia fedha zaidi katika utafiti na tiba.

Tangu wakati huo mamilioni ya dola yamekuwa yakitolewa kila mwaka, na mamia ya mamilioni ya dozi za kinga na dawa vimewanufaisha watu wengi.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio yaliyoelezwa katika ripoti ya WHO kuhusu mapambano dhidi ya magonjwa hayo ya kitropiki, shirika hilo limeonya kuwa juhudi hizo zinaweza kukwama, ikiwa hapatakuwepo mafanikio katika vita dhidi ya umasikini.

Makadirio ya WHO yanaonyesha kuwa wapo watu zaidi ya bilioni 2.4 duniani ambao hawana huduma za msingi za afya na usafi, kama vile vyoo, na kwamba watu bilioni mbili bado wanakunywa maji yenye chembechembe zitokanazo na kinyesi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW