1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

WHO: Hospitali za Rafah kukosa mafuta ndani ya siku tatu

9 Mei 2024

Shirika la Afya Duniani WHO limesema akiba yake ya mafuta iliyosalia kule Rafah inaweza kufanikisha operesheni zake kusini mwa Gaza kwa siku tatu zijazo pekee.

Mzozo wa mashariki ya Kati | Rafah
Wapalestina waendelea kuondoka maeneo ya mashariki mwa Rafah kufuatia mashambulizi ya Israel.Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Hayo yakijiri Ripoti zinasema Israel imefanya mashambulizi ndani ya Rafah licha ya onyo la Marekani kwamba litasita kuipa Israel silaha zake ikiwa itaendelea na mpango wake wa operesheni ya kijeshi Rafah. 

Tayari upungufu huo wa mafuta umesababisha hospitali moja kati ya tatu zinazohudumu mjini Rafah kufunga milango yake.

Kivuko cha Rafah kati ya Gaza na Misri kimefungwa tangu Israel ilipochukua udhibiti wa upande wa Palestina mapema Jumanne, na kuzuia misaada ya kiutu inayohitajika mno kuingizwa Gaza.

Umoja wa Mataifa umesema upande wa kaskazini mwa Gaza tayari uko katika hali ya kile ulichokiita "njaa kamili”. Katika siku chache zilizopita, Wapalestina wamekuwa wakiukimbia mji wa Rafah kabla ya mashambulizi ya ardhini.

Je kivuko cha Shalom kimefunguliwa?

Israel ilisema ilifungua tena kivuko cha Shalom siku ya Jumatano, kuruhusu misaada kuingizwa Gaza. Lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema hakuna msaada ambao umepokelewa upande wa Wapalestina kwa sababu ya mapigano yanayoendelea.

Soma pia:Israel yafungua tena kivuko mpakani kati ya Gaza na Misri

Vita vinavyoendelea Gaza vimesababisha asilimia 80 ya idadi jumla ya wakaazi milioni 2.3 kuyakimbia makaazi yao. Vimeharibu majumba ya watu na kusababisha uharibifu mkubwa wa makaazi, hospitali, misikiti, shule na miundo mbinu katika miji kadhaa.

Kulingana na wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya vifo katika ukanda huo imepita 34, 500.

Vita vya Gaza vilianza Oktoba 7, baada ya wanamgambo wa Hamas kufanya shambulizi baya kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1, 200. Aidha wanamgambo wa Hamas waliwashika mateka karibu watu 250 na kuwapeleka Gaza. Israel inasema wanamgambo hao bado wanawashikilia takriban mateka 100, na miili ya zaidi ya mateka 30.

Soma pia:Mashaka yagubika operesheni ya Israel mji wa Rafah

Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa nchi ambazo zimeliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Mashambulizi yaripotiwa Rafah

Hayo yakijiri, Israel imefanya mashambulizi Alhamisi mjini Rafah mnamo wakati rais wa Marekani Joe Biden akitoa onyo kali na kuahidi kuacha kuipa Israel silaha ikiwa itaendelea mbele na mpango wake wa operesheni ya kijeshi katika mji huo wa kusini mwa Gaza.

Rais wa Marekani Joe Biden ametishia kutopia Israel silaha ikiwa itaendelea na mpango wake wa kushambulia Rafah.

Waandishi wa shirika la habari la AFP wameripoti kwamba kumetokea mashambulizi makali asubuhi ya Alhamisi. Kwa mujibu wa shirika hilo la Habari, muda mchache baadaye jeshi la Israel lilisema linashambulia ngome za wanamgambo wa Hamas eneo la kati ya Ukanda wa Gaza.

Soma pia: Israel yawaamuru maelfu ya Wapalestina kuondoka Rafah

Israel tayari ilishapeleka vifaru vya kivita katika mji huo wa mpakani na kufanya mashambulizi maalum dhidi ya maeneo inayosema ni ngome za vikosi vilivyosalia vya Hamas. Lakini maeneo hayo pia yamejaa raia wa Kipalestina waliokimbia vita kwingineko.

Mnamo Jumatano, rais wa Marekani Joe Biden alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha CNN, alionya kwamba atachelea kuipa Israel silaha za Marekani ikiwa itaendelea mbele na mpango wake wa mashambulizi ya ardhini ndani ya mji wa Rafah. Biden alikiri kuwa mabomu ya Marekani yamewaua Wapalestina kufuatia vita vinavyoendelea Gaza.

Israel imetaja onyo hilo la Biden kuwa la kukatisha tamaa sana.

Vyanzo: APE, AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW