WHO: Janga la COVID-19 lazidi kuwa baya ulimwenguni
14 Julai 2020Mkuu wa shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameonya kwamba janga la COVID-19 linaendelea kuwa baya zaidi ulimwenguni kote. Tedros ameongeza kwamba japo nchi nyingi haswa za barani Ulaya na Asia zimefanikiwa kulidhibiti janga hilo, katika mataifa mengine maambukizi yanazidi kuongezeka na yamechukua njia mbaya.
Akizungumza na waandishi wa habari, Tedros amesema hali ya kawaida haitarejea hivi karibuni.
Kauli ya Tedros imejiri mnamo wakati idadi ya maambukizi ya virusi vya corona imepindukia watu milioni 13 ulimwenguni, na zaidi ya watu 570,000 wamefariki, huku Marekani ikiendelea kurekodi idadi ya juu ya maambukizi mapya. Bila ya kumtaja yeyote jina, Tedros amewashutumu viongozi wa kisiasa wanaotoa kauli zinazokanganya kuhusu janga hilo.
Muda bado upo wa kuzuia virusi vya corona
"Wacha niseme bayana. Nchi nyingi zinaelekea njia mbaya. Kirusi hiki kinasalia kuwa adui wa umma, lakini matendo ya serikali na watu hayaakisi haya. Lengo pekee la kirusi ni kupata watu wa kuambukiza." Amesema Tedros.
Amezitaka nchi kuweka mkakati kabambe wa kukabili idadi inayozidi kuongezeka ya maambukizi mapya, huku akisema kuwa nusu ya jumla ya maambukizi mapya hutokea mataifa ya Amerika.
Hata hivyo Tedros amesema bado kuna njia ya kulishughulikia janga la corona na kwamba muda hauujatupa kisogo wa kuudhibiti hata katika maeneo ambayo yamekuwa na maambukizi mengi.
California laweka tena vizuizi
Kwingineko nchini Marekani, jimbo la California limefuta mipango yake ya kulegeza masharti yaliyowekwa ya kukabiliana na virusi hivyo hatari. Hatua hiyo imejiri kufuatia ongezeko la idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya corona katika jimbo hilo na majimbo kadhaa nchini Marekani.
Gavana wa California Gavin Nesom ameamuru mikahawa yote pamoja na mabaa na kumbi za filamu kufungwa tena.
Katika jimbo hilo tajiri zaidi na lenye idadi kubwa zaidi ya watu Marekani; makanisa, maeneo ya ndani ya kufanyia mazoezi pamoja na maduka makubwa, ambayo huduma zao si muhimu pia yametakiwa kusitisha shughuli zao za ndani katika nusu ya jimbo hilo ambalo limeathiriwa zaidi.
Jimbo la California lilikuwa la kwanza kutangaza amri ya kusalia majumbani. Mnamo mwezi Mei, liliruhusu biashara kadhaa kufungua, lakini sasa ongezeko la idadi ya maambukizi limelilazimisha kurejesha tena vizuizi.
Tedros amesema hali nne tofauti sasa zinajitokeza ulimwenguni. Nazo ni nchi ambazo zimekuwa chonjo na zilizuia mripuko kwa kiwango kikubwa, zile ambazo zimeweza kudhibiti miripuko ya kiwango kikubwa, zile ambazo zililegeza masharti na sasa maambukizi yameanza tena kurudi na zile ambazo ndizo sasa zinakabiliwa na maambukizi mapya kwa wingi.
Chanzo: AFPE
Mwandishi. John Juma
Mhariri: