1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Kifua kikuu ndiyo ugonjwa hatari zaidi wa maambukizi

25 Machi 2020

Wakati vifo vinavyotokana na virusi vya corona vikiongezeka duniani, maafisa wa afya ulimwenguni wanakumbusha kuwa kifua kikuu ni ugonjwa hatari zaidi duniani.

Multiresistente Tuberkulose in der Ukraine
Picha: DW

Zaidi ya vifo milioni moja vinaripotiwa kila mwaka. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ugonjwa wa kifua kikuu unawaua watu wengi zaidi kuliko ugonjwa mwingine wowote ule wa kuambukiza. Takriban watu milioni 1.5 walikufa kutokana na ugonjwa huo wa maambukizi ya bakteria mwaka 2018.

Shirika la Afya Duniani, WHO, limekumbusha hilo katika kuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani ambayo huadhimishwa kila Machi 24. Karibu watu milioni 10 wanaambukizwa kifua kikuu kila mwaka na idadi ndogo tu ya visa hivyo wanapatiwa dawa muhimu za kuokoa maisha.

WHO imeeleza kuwa zaidi ya watu 4,000 wanakufa kwa kifua kikuu kila siku. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema janga la virusi vya corona lililopo sasa, linaonyesha jinsi wagonjwa wenye matatizo ya mapafu au wenye kinga dhaifu wanavyoathirika na mripuko wa virusi hivyo. Kifua kikuu ni ugonjwa ambao kimsingi unaathiri mapafu.


Mgonjwa wa kifua kikuu nchini Kenya akikagua dawa zake katika kliniki ya kudhibiti kifua kikuu inayosimamiwa na shirika la Madaktari wasio na Mipaka, MSF.Picha: picture-alliance/epa/D. Irungu

''Kwa mamilioni ya watu wanaougua kifua kikuu, virusi vya corona vinaashiria hatari kubwa kwa sababu tayari mapafu yao yamedhoofika kutokana na ugonjwa huo, afya yao kwa ujumla ni duni kwa sababu ya umasikini na hawawezi kupata huduma nzuri za afya,'' anasema Burkard Kömm, mkurugenzi wa shirika la Ujerumani linaloshughulikia magonjwa ya ukoma na kifua kikuu, DAHW.

Barani Asia na Afrika, ni wagonjwa wa kifua kikuu ndiyo wana uwezekano mkubwa wa kufa kutokana na virusi vya corona. Shirika la DAWH, limebainisha kuwa mgonjwa wa kifua kikuu anaweza kupona iwapo atapatiwa matibabu ya miezi sita ya mchanganyiko wa dawa za aina nne za kupambana na maradhi yanayosababishwa na vimelea za antibiotiki.

Hata hivyo, wagonjwa wengi wanamaliza tiba zao mapema au dawa zinashindwa kufanya kazi hatua ambayo inaleta changamoto na kumfanya mgonjwa aongeze muda wa matibabu.

Shirika la DAWH limefafanua kwamba ukosefu wa dawa pia ni sababu kuu ambayo inasababisha wagonjwa kumaliza matibabu yao mapema.

Chnazo: EPD, DPA

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW