WHO kuanza majaribio ya chanjo ya Ebola
22 Oktoba 2014Mkuu wa kitengo cha habari cha WHO Marie Paule Kieny, amesema tayari mashirika yanayoshirikiana na shirika lao yameanza kuandaa vituo vya matibabu katika nchi tatu zilizoathiriwa zaidi na maradhi ya Ebola, ambazo ni Guinea, Liberia na Sierra Leone. Amesema pia kwamba makampuni ya kutengeneza madawa yanazifanyia majaribio dawa na chanjo za Ebola moja kwa moja huko Afrika Magharibi, kama yalivyoshauriwa na WHO pamoja na wataalamu wa kimataifa.
Afisa huyo amethibitisha kwamba maelfu ya vipimo vya dawa ya chanjo ya majaribio dhidi ya Ebola yataanza kutolewa kwa wahudumu wa afya, na pengine kwa watu wanafanya kazi ya kuwazika wahanga wa Ebola huko Afrika Magharibi.
''Majaribio ya chanjo zote mbili yataanza wiki mbili zijayo, na tunategemea kuwa matokeo ya awali ya chanjo hizo; nasema ya awali kwa sababu majaribio yataendelea kwa muda wa kati ya miezi sita na mwaka mmoja, lakini matokeo kuhusu ufanisi wa chanjo zenyewe, usalama wake na kipimo mahsusi cha dawa kwa kila chanjo, yatajulikana ifikapo Desemba''. Amesema Kieny.
Shughuli kwenye maabara
Dawa inayojaribiwa ina kingamwili ambazo zinaweza kumsaidia mgonjwa kuvishinda virusi vya ugonjwa wa Ebola. Hata hivyo bado dawa hiyo inafanyiwa kazi katika maabara.
Afisa wa WHO amesema kila hatua ya usalama inapaswa kuchukuliwa kuhakikisha usalama wa watu wanaotoa damu yao kutumiwa katika dawa hiyo, na pia usalama wa wale watakaoipokea. Na wakati huo shirika la atomiki la Ufaransa limesema kuwa limetengeneza zana ambazo zinaweza kugundua virus vya ebola katika damu na mkojo vya mgonjwa katika muda wa dakika 15. Kawaida shughuli hiyo huchukua saa kadhaa.
Katika juhudi hizo hizo za kupambana na maradhi ya Ebola, shirika la msalaba mwekundu la Ujerumano, DRK, limetoa wito kwa watu kujitolea kushiriki katika mapambano hayo, lakini miongoni mwa wapatao 483 waliojitokeza, 196 tu ndio wenye sifa zinazohitajika.
Idadi ya waliojitolea haitoshi
Rais wa shirika hilo Rudolf Seiters ameliambia gazeti la kila siku la Die Welt kwamba idadi hiyo haitoshi kabisa kuiendesha kliniki ya kutibu Ebola, akisema inabidi kubadilisha wafanyakazi kila baada ya wiki nne ili kupunguza uwezekano wa kuambukiza ugonjwa huo.
Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na shirika la msalaba mwekundu la nchi hiyo iko katika mchakato wa kuanzisha vituo vya matibabu ya Ebola nchini Liberia na Sierra Leone. Wiki iliyopita Ujerumani ilizidisha mara sita kiwango cha fedha ilichokuwa ikichangia katika juhudi za kimataifa dhidi ya Ebola, na kufikia Euro milioni 102.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank Walter Steimeier amesema dunia imejikokota sana katika kuukabili ugonjwa wa Ebola, na kwamba huu ni wakati wa kufidia muda uliopotea.
Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/DPAE/DW website
Mhariri:Hamidou Oumilkheir