WHO kuzifanyia utafiti dawa za mitishamba juu ya COVID-19
22 Julai 2020Jopo hilo jipya la ushauri litaunga mkono nchi katika majaribio ya kitabibu, utafiti mwingine na utengenezaji wa dawa nyingine za kienyeji wakati hivi sasa janga likisambaa kwa kasi katika baadhi ya sehemu za bara la Afrika. Kesi zilizothibitishwa katika bara hilo zimekaribia kufika 750,000, zaidi ya nusu zikiorodheshwa nchini Afrika kusini.
Taarifa ya WHO imesema dawa za asili, zina faida nyingi na bara hilo lina historia ndefu ya matumizi yake. Mkuu wa WHO barani Afrika Matshidiso Moeti amesema utafiti unapaswa kuwekwa katika misingi ya kisayansi.
Mataifa kadhaa yalionesha shauku baada ya rais wa Madagascar kutangaza dawa ya mitishamba kama sehemu ya taifa hilo la kisiwani kupambana na janga la virusi vya corona.
Maambukizi duniani
Maambukizi ya virusi vya corona duniani yameongezeka kupindukia watu milioni 15 kufikia siku ya Jumatano, kwa mujibu wa idadi iliyowekwa pamoja na shirika la habari la Reuters, wakati ugonjwa huo ukishika kasi hata wakati nchi bado zinaendelea kutofautiana katika jibu lao dhidi ya janga hilo.
Nchini Marekani, nchi ambayo ina idadi kubwa ya maambukizi duniani ikiwa na watu milioni 3.91 ya walioambukizwa, rais Donald Trump alionya, kuwa huenda hali itakuwa mbaya zaidi kabla ya kutengemaa.
Nchi tano za juu ambazo zina maambukizi makubwa ni pamoja na Brazil, India, Urusi na Afrika kusini. Lakini idadi iliyowekwa pamoja na shirika la habari la Reuters inaonesha ugonjwa huo unasambaa kwa kasi katika mataifa ya Amerika, ambayo yana zaidi ya nusu ya maambukizi duniani kote na nusu ya vifo. Duniani kote pia kiwango cha maambukizi hakioneshi ishara ya kupungua kasi.