1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO kuzindua uchunguzi wa madai ya ngono DRC

13 Oktoba 2021

Wafadhili wakuu wa nchi za Magharibi wamelisisitizia Shirika la Afya Ulimwenguni WHO kuzindua uchunguzi wa kina zaidi wakidai juu kashfa kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia nchini Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo.

 (WHO) Generaldirektor Tedros Adhanom Ghebreyesus
Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: MOHAMED AZAKIR/REUTERS

Kulingana na Tume Huru nchini Congo, Baadhi ya wafanyikazi wa misaada 83, robo yao wakiwa wameajiriwa na shirika la WHO, walihusika katika unyanyasaji wa kijinsia wakati wa janga la Ebola kutoka mwaka 2018 hadi 2020.

Wanawake waliwashtumu wafanyikazi wa misaada wa ndani na wa kigeni kudai ngono ili kupata ajira na kulikuwa na madai tisa ya ubakaji, haya ni kwa mujibu wa ripoti ya jopo la tume huru juu ya unyanyasaji mkubwa huko Kivu Kaskazini na majimbo ya Ituri.

Wanadiplomasia wamesema, Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus na wasaidizi  wake wametoa rasimu ya mpango wa utekelezaji utakaojumuisha wafadhili wakuu ambao ni pamoja na Marekani, Uingereza, mamlaka ya Ulaya, Canada na Australia huku wakitoa wito wa kutaka uchunguzi uendeshwe na jopo la nje wakati WHO pia inarekebisha sera za ndani.

Uchunguzi huo unapaswa kuchunguza jinsi usimamizi wa shirika la WHO ulivyoshughulikia kuongezeka kwa madai ya unyanyasaji pamoja na lengo la kuanzisha uwajibikaji kwa watuhumiwa.

Hatua madhubuti

Picha: Reuters/G. Tomasevic

Mpango wa usimamizi, kwa sasa unarekebishwa na unatarajiwa kuwasilishwa kwa nchi 194 wanachama wa WHO mnamo Alhamisi, na unapaswa kuweka hatua madhubuti na kutambua udhaifu katika usimamizi ili kuzuia unyanyasaji wa baadaye katika operesheni za dharura.

Awali Mkurugenzi wa Shirika la Afya Dunia WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus aliahidi kuchukua jukumu kuhahikisha kwamba wahusika watawajibishwa.

"Ni kipaumbele changu cha juu kuhakikisha kuwa wahusika hawaachiwi huru, lakini wanawajibishwa . Kama mkurugenzi nabeba dhamana kwa tabia ya watu tunaowaajiri, na kwa kasoro yoyote katika mifumo yetu ambayo iliruhusu tabia hii. Nitabeba dhamana la kibinafsi kwa kufanya mabadiliko yoyote tunayohitaji kufanya ili kuzuia tabia hii kutokea baadaye "

Aidha mwanadiplomasia mwengine amedokeza kwamba ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Huduma za Usimamizi wa Ndani (OIOS) itakuwa mstari wa mbele kuongoza uchunguzi huo ambao unapaswa kupata njia ya kuhakikisha uwajibikaji unatekelezwa kwa uzito unaohitajika.

 

Vyanzo: Reuters, EBU