1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Maambukizi ya virusi vya corona yaongezeka ulimwenguni

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
13 Julai 2020

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO limethibitisha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona kote ulimwenguni. Jumla ya watu 230,370 wameambukizwa katika muda wa saa 24.

Spanien Palma de Mallorca | Coronavirus | Touristen am Strand
Picha: Reuters/E. Calvo

Shirika la Afya duniani WHO limesema nchi zilizoathirika zaidi ni Marekani, Brazil, India na Afrika Kusini. Marekani ndio inayoongoza kwa kuwa na idadi ya watu wapatao elfu 66,500 walioambukizwa katika muda wa saa 24. Kulingana na taarifa ya Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, zaidi ya watu milioni 12.7 kote ulimwenguni wamethibitishwa kuwa wanaugua COVID-19 wakati ambapo zaidi ya watu 565,000 wamekufa. Hata hivyo, zaidi ya watu milioni saba waliokuwa wanaugua COVID -19 wamepona.

Wakati huo huo, utawala wa rais wa Marekani Donald Trump unashinikiza kufunguliwa kwa shule licha ya kuzidi kuongezeka maambukizi ya corona na idadi ya wagonjwa wa COVID-19 nchini humo hatua ambazo zimezusha ukosoaji mkubwa na kuleta wasiwasi kwamba kwa watoto kurudi madarasani inaweza kusababisha hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo.

Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens SpahnPicha: Reuters/F. Bensch

Afrika Kusini imerejesha karantini kuanzia jana Jumapili. Rais Cyril Ramaphosa amesema nchi yake inakabiliwa na dhoruba kali ya janga la corona ambalo ni baya kuwahi kutokea. Eneo la Catalonia nchini Uhispania limewarudisha maelfu ya watu kwenye karantini huku maambukizi ya corona yakiendelea kuongezeka katika sehemu nyingi za ulimwengu.

Ujerumani mpaka sasa imeweza kudhibiti maambukizi, idadi ya watu walioambukizwa ni 200,000 na watu 9,071 wamekufa hadi sasa. Hata hivyo, Waziri wa Afya Jens Spahn amewataka Wajerumani kuwa macho ili kuzuia wimbi la pili la maambukizi. Spahn aliwaambia waandishi wa habari kwamba amesikitishwa na Wajerumani wanaofanya likizo kwa papara baada ya kukaa kwenye karantini kwa miezi kadhaa, amewataka wajiepushe na tabia zinazoweza kuwaletea madhara wanapokuwa likizoni.

Virusi vya corona vimesababisha mgongano baina ya wataalam wa afya juu ya maelezo sahihi kuhusiana na jinsi maambukizi yanavyoweza kuenezwa. Shirika la Afya Ulimwenguni limekiri wiki hii kwamba virusi vya corona vinaweza kuenea kupitia matone madogo madogo yaliyo kwenye hewa, wanasayansi zaidi ya 200 awali walikuwa wamelalamika kwamba WHO imeshindwa kutoa tahadhari kwa umma juu ya hatari hii.

Huko nchini India na ulimwenguni kote mashabiki wa mcheza filamu mashuhuri Amitabh Bachchan, mwenye umri wa miaka 77, aliyethibitishwa kuugua COVID-19 mnamo siku ya Jumamosi na kulazwa hospitalini mjini Mumbai wanaendelea kumtakia afueni ya haraka. Amitabh Bachchan na mwanawe wote wameambukizwa virusi vya corona. Imeripotiwa kuwa hawamo kwenye hali mahututi.

Vyanzo:/AFP/AP/RTRE/

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW