1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Mapambano dhidi ya malaria yakwama.

29 Novemba 2017

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, limesema mafanikio ya mapambano dhidi ya malaria duniani yamekwama, huku kukiwa na dalili za kutoongezwa kwa ufadhili na kutochukuliwa kwa ugonjwa huo kuwa ni kitisho tena. 

USA Stechmücke Anopheles quadrimaculatus in Miami
Picha: picture-alliance/dpa/US CfDCaP/EFE

Ripoti iliyotolewa leo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, imeeleza kuwa mafanikio katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria duniani yamekwama, wakati ambapo kuna dalili za kutoongezwa kwa ufadhili na kutochukuliwa kwa ugonjwa huo unaoenezwa na mbu kuwa kitisho tena. 

Shirika hilo limesema kwenye ripoti yake ya mwaka iliyotolewa leo kwamba ugonjwa wa Malaria umeathiri kiasi ya watu milioni 216 katika nchi 91 kwa mwaka 2016, ikiwa ni ongezeko la visa milioni 5, vilivyotokea mwaka uliopita. Malaria imeua watu 445,000, idadi inayokaribiana na ile ya mwaka 2015.

Kulingana na Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la afya, Tedros Adhanom Ghebreyesus kiwango hiki kinaashiria wasiwasi wa kutofikiwa kwa malengo ya mwaka 2020 ya shirika hilo chini ya Mkakati wake wa kimatiafa wa kukabiliana na malaria wa Global Strategy for Malaria. Ameongeza kuwa hata kwa nchi zilizopiga hatua hapo nyuma hivi sasa zinarudi nyuma.

Idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na malaria ni vya watoto walio chini ya miaka mitano katika mataifa masikini zaidi yaliyoko kusini mwa Jangwa la Sahara.  Kwa mujibu wa Tedros, asilimia 90 ya visa na vifo vya malaria duniani kote hutokea barani Afrika. Mataifa 15, kasoro moja yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara yamebeba asilimia 80 ya mzigo wa malaria, huku akitoa mwito wa kulitia maanani suala la kuzisaidia zaidi nchi zinazoathirika zaidi. 

Watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wanaongoza kwa idadi ya vifo vitokanavyo na malaria kusini mwa Jangwa la SaharaPicha: Getty Images/S.Jensen

Mtaalamu kutoka shirika la WHO anahusika na Malaria na kiongozi wa jopo lililoandaa ripoti hiyo Abdisalan Noor amesema "baada ya kipindi cha mafanikio makubwa, hatupigi hatua yoyote tena. Amesema "Nina wasiwasi na namna tulivyoridhika".

Kutoongezeka kwa ufadhili wa kifedha kunazidi kudidimiza mapambano dhidi ya malaria.

Mkurugenzi wa mpango wa kimataifa wa malaria wa WHO Pedro Alonso amesema kwa sehemu hali hii inatokana na ufadhili, na kwa sehemu nyingine ni kutokana na namna serikali zilivyoamua kulichukulia suala la malaria, na ndio maana mafanikio yaliyoonekana muongo uliopita hayaendelezwi tena.

Ufadhili jumla unaotolewa katika mapambano dhidi ya malaria haujaongezwa tangu mwaka 2010. Mwaka 2016, karibu Dola bilioni 2.7 ziliwekezwa katika juhudi za kukabiliana na kuutokomeza ugonjwa wa malaria duniani. Mwaka 2015, fedha zilizotolewa zilifikia dola bilioni 2.9, kiasi kilichokaribiana na kilichotolewa mwaka 2010. 

Ripoti hiyo ya WHO imegundua kwamba kiwango hicho cha fedha kinaponyambuliwa kwa nchi na nchi kwa kuzingatia msingi wa kipato cha mtu mmoja mmoja, ni dhahiri kwamba fedha zinazopelekwa katika nchi zinazotishiwa zaidi na malaria zimepungua kwa wastani wa chini ya dola 2 kwa mwaka kwa kila mtu anayekabiliwa na kitisho cha malaria.

Noor amesema, pamoja na kutoongezeka kwa ufadhili, ripoti hiyo pia imegundua kuwepo kwa pengo katika upatikanaji na matumizi ya zana muhimu za kuzuia malaria, vifaa vya uchunguzi na matibabu kama vile vyandarua, dawa za kupulizia ndani ya nyumba na huduma za msingi za afya.

Ni makazi machache katika mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara yaliyo na vyandarua vya kutosha vya kujilinda na kung'atwa na mbu, na takriban theluthi ya watoto barani Afrika walio na homa wanaoweza kupata huduma za bure katika vituo vya afya vya umma.

Amesema asilimia 90 ya visa na vifo vya malaria duniani kote vinatokea barani Afrika . Mataifa 15, kasoro moja yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara yamebeba asilimia 80 ya mzigo wa malaria, na kwamba ili kuirejesha dunia katika hatua ya awali, suala la kuzisaidia zaidi nchi zinazoathirika zaidi linatakiwa kupewa uzito mkubwa. 

Mwandishi: Lilian Mtono/ECA/RTRE/WHO.

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW