1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Chanjo ya pili ya malaria ipo tayari kwa matumizi

3 Oktoba 2023

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limeridhia chanjo ya pili ya ugonjwa wa malaria kwa watoto, ambayo inaweza kuokoa maisha ya maelfu endapo kutakuwa na uwezekano wa kuziba pengo kubwa la usambazaji na mahitaji.

Südafrika | Eröffnung Zentrum für mRNA-Impfstoffproduktion und Technologietransfer in Kapstadt | Tedros Adhanom
Picha: Esa Alexander/REUTERS

Takriban watoto nusu milioni katika kanda ya Afrika hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo unaosababishwa na vimelea vinavyoenezwa na mbu.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus amenukuliwa akiseama "Kama mtafiti wa malaria, nilikuwa na ndoto ya siku ambayo tutakuwa na chanjo salama na yenye ufanisi dhidi ya malaria. Sasa tuna mbili."

Burkina Faso, Ghana na Nigeria zitakuwa za mwanzo kuitumia

Chanjo mpya ya R21/Matrix-M, iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza na kuzalishwa na taasisi ya Serum ya India, tayari imeidhinishwa kutumika nchini Burkina Faso, Ghana na Nigeria.

Mtoto akiwa na wazazi wake huko Brazil katika jitihada ya kumnusuru akihusishwa na maradhi ya malaria.Picha: Edmar Barros/AP/picture alliance

Mwaka 2021, chanjo ya RTS,S, iliyotolewa na kampuni kubwa ya dawa ya Uingereza GSK, ilikuwa ya kwanza kupendekezwa na WHO katika kudhibiti ugonjwa wa Malaria kwa watoto katika maeneo yenye maambukizi ya wastani hadi ya juu.

Tedros anasema kumekuwa na uhitaji mkubwa wa chanjo ya RTS,S, kwa hivyo chanjo hii ya sasa ya nyongeza itakuwa hatua muhimu katika kuwalinda watoto kwa haraka zaidi, na itawaleta pamoja katika ile dira ya kutokomeza kaibsa malaria.

Chanzo ina nafasi kubwa ya kupunguza athari za malaria Afrika

Takriban nusu ya idadi ya watu duniani inaishi katika maeneo yenye hatari kubwa ya malaria, huku visa vingi na vifo vikitokea barani Afrika. Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dokta Matshidiso Moeti, amesema chanjo hiyo mpya ina uwezo mkubwa kwa bara hilo kwa kusaidia kuziba pengo kubwa la mahitaji na usambazaji.

Tangu mwaka 2019, mipango ya majaribio ya kuanzisha chanjo ya RTS,S katika nchi tatu -- Ghana, Kenya na Malawi -- imewezesha watoto milioni 1.7 kupata angalau dozi moja.Mipango hii imesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa aina kali na mbaya za malaria, na kupunguza kwa vifo vya watoto.

WHO imesema angalau nchi 28 za Afrika zinapanga kuanzisha matumizi ya chanjo hiyo mpya ya malaria iliyopendekezwa ikiwa kama sehemu ya programu zao za kitaifa za chanjo. Imeongeza kwa kusema  kuwa chanjo ya RTS,S itapelekwa katika baadhi ya nchi za Afrika mapema 2024, na chanjo ya R21 inatarajiwa kupatikana katikati ya 2024.

Soma zaidi:India yaweka vizuizi baada ya kirusi cha Nipah kuuwa watu 2

Chanjo hizi mbili zina viwango sawa vya ufanisi vya karibu asilimia 75. Ufanisi wa chanjo hiyo mpya ungelinganishwa na chanjo nyingine za utotoni, huku dozi ya R21/Matrix-M ikigharimu kati ya $2 na $4.

Taarifa wa wadau wa chanjo inasema WHO na washirika wake wametoa maombi ya dozi milioni 60 ifikapo mwaka 2026. Kiwango hicho kinatarajiwa kuongezeka na kufikia dozi milioni 100 ifikapo 2030.

Chanzo:RTR

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW