1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Tanzania inaficha taarifa za uwepo wa Ebola

Angela Mdungu
23 Septemba 2019

Shirika la afya duniani WHO limesema Tanzania inakataa kutoa maelezo ya kina juu ya tetesi za kuwepo kwa visa vya homa ya Ebola nchini humo

Michael Ryan Geschäftsführer WHO
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Trezzini

WHO imesema uwazi na kasi ya kukabiliana na mlipuko wa homa hiyo ni muhimu kwani inaweza kusambaa kwa haraka. Taarifa ya Shirika la Afya duniani iliyotolewa mwishoni mwa juma imesema shirika hilo lilijulishwa mnamo Septemba 10 juu ya kifo cha mgonjwa mmoja mwanamke jijini Dar es salaam na kwamba taarifa zisizo rasmi zilisema, vipimo vyake vilionesha alikuwa na virusi vya Ebola.

Taarifa hiyo imesema watu waliokutana na mgonjwa huyo wamewekwa karantini katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Tanzania ilitoa kauli rasmi wiki iliyopita ikithbitisha kuwa hakuna visa wala wagonjwa wanaodhaniwa kuwa na homa ya Ebola. Serikali ya nchi hiyo haikuzungumzia moja kwa moja juu ya kifo cha mwanamke anayedaiwa kufa kwa Ebola wala kutoa maelezo zaidi. 

Licha ya kuwasilisha maombi kadhaa kwa serikali ya Tanzania, WHO imesema haijapokea taarifa za hospitali, majibu ya vipimo, na vipimo muhimu vya maabara pamoja na watu waliokuwa na muingiliano na mgonjwa huo.

Waziri wa Afya wa Marekani Alex AzarPicha: Reuters/K. Lamarque

Taarifa ya Shirika la afya duniani, juu ya uwezekano wa kuwepo kwa homa ya Ebola nchini Tanzania, imetolewa baada ya  Waziri wa afya wa Marekani Alex Azar kuikosoa Tanzania wiki iliyopita kwa kushindwa kutoa taarifa juu ya uwezekano wa kuwepo kwa homa ya Ebola nchini humo.

WHO iko tayari kufanya kazi na Tanzania kama itaombwa kufanya hivyo

Akizungumzia suala hilo, Azar Alisema WHO ina wasiwasi  juu ya kutokuwepo kwa uwazi kuhusu kifo cha kwaza na inatoa wito kwa serikali ya Tanzaniakuwa wazi na kutoa majibu ya maabara pamoja na taarifa zinazomhusu mtu huyo.  Amesema, WHO inaendelea kufanya kazi kuhakikisha Tanzania inazingatia taratibu za  kimataifa za afya na jukumu lake kwa Shirika la afya duniani na nchi nyingine wanachama.

Kwa upande wake msemaji wa WHO Tarik Jasarevic amesema shirika  hilo liko tayari kuisaidia Tanzania iwapo itathibitika kuwepo kwa mlipuko wa Ebola na kama Serikali ya Tanzania itaomba kusaidiwa.

Mamlaka za Mashariki mwa Afrika na Afrika ya Kati zimekuwa katika hali ya tahadhari baada ya uwezekano wa kusambaa kwa homa ya Ebola kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo Ugonjwa huo kwa mwaka mzima, umeua zaidi ya watu 2,000.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW