1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu watolewa wito wa kubadilisha lishe na kufanya mazoezi

Mjahida6 Aprili 2016

Shirika la afya duniani WHO limesema Idadi ya watu wanaokadiriwa kuishi na ugonjwa wa kisukari imeongezeka mara nne zaidi ndani ya miaka 35 iliyopita.

12.11.2015 DW fit und gesund Diabetes_Teaser
Kisukari

Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa limesema idadi ya watu wazima wanaoishi na kisukari imeongezeka kufikia watu milioni 422 mwaka wa 2014 ikilinganishwa na watu milioni 108 mwaka wa 1980. Ongezeko hilo linadaiwa kusababishwa na namna watu wanavyokula, kuishi pamoja na mfumo wao wa mazoezi kuwa mdogo.

Katika ripoti yake ya kwanza juu ya ugonjwa huo wa kisukari shirika hilo la WHO limesema mwaka wa 2012 ugonjwa huo uliripotiwa kusababisha vifo vya watu milioni 1.5 duniani, huku vifo vinavyotokana na kupanda kwa viwango vya sukari mwilini vinavyofungamanishwa na kisukari vikiripotiwa kufikia watu milioni 2.2 mwaka huo huo wa 2012.

"Ugonjwa wa kisukari ndio moja ya ugonjwa unaoua watu wengi duniani kwa sasa," alisema Etienne Krug, anayeongoza kitengo kinachoshughulika na uitikiaji wa ugonjwa huo katika shirika la WHO.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO Margaret ChanPicha: picture-alliance/dpa/S. di Nolfi

Aidha eneo lililoathirika sana kwa kuwa na visa milioni 131 vya ugonjwa huo mwaka 2014 ni eneo la pasifiki ya Magharibi linalojumilisha mataifa kama Japan na China, eneo la pili ambalo ni Kusini Mashariki mwa Asia linalojumuisha maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu kama India na Indonesia wana visa milioni 96 vya ugonjwa huo.

Huku Ulaya na Amerika wakishika nafasi za tatu na nne katika orodha hiyo wakiwa na visa milioni 64 na milioni 62 vya ugonjwa wa kisukari.

Ugonjwa huo umegawika katika aina mbilii. Hakuna njia ya kukwepa aina ya kwanza ambapo inatokea pale kongosho au Pancrease kwa lugha ya kingereza inaposhindwa kutengeneza homoni ya insulin inayodhibiti viwango vya sukari kwenye damu, na wale wanaoishi na aina ya pili ya ugonjwa huo inafungamanishwa na uzito kupita kiasi, namna mtu anavyoishi, na hii inaweza kuepukika kwa watu wazima na watoto kuzingatia lishe bora na kufanya mazoezi.

WHO inapendekeza watu wazima kuanzia miaka 18 hadi 65 kufanya mazoezi ya angalau dakika 150 kwa wiki ikiwa ni pamoja na shughuli za kimwili kama vile kukimbia na kutembea.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Iddi Ssesanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW