WHO: Vifo vitokanavyo na Malaria vimepungua
9 Desemba 2015Ripoti mpya ya Shirika la Afya Ulimwenguni inaonyesha kwamba vifo vilivyotokana na ugonjwa wa Malaria vimeshuka hadi 438,000 mnamo mwaka huu wa 2015, ikiwa ni idadi ndogo ikilinganishwa na mwaka 2000, ambapo watu 839,000 waliuawa na Malaria. Aidha, kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi ambazo zinaelekea kuutokomeza ugonjwa wa Malaria zimeongezeka.
WHO inaeleza katika ripoti yake kwamba katika muda wa miaka 14 iliyopita, mikakati ya kupambana na ugonjwa huo katika nchi nyingi za Afrika, ikiwemo matumizi ya vyandarua vitandani na kupuliza dawa ya kuuwa wadudu nje na ndani ya nyumba imeokoa mamilioni ya maisha ya watu, na fedha nyingi ambazo zingetumiwa kuwatibu wagonjwa.
Ingawa nchi za Afrika zinaendelea kuongoza kwa idadi ya watu wanaokufa kwa Malaria, tangu mwaka 2000 nchi hizo zimeshuhudia kupungua kwa vifo hivyo kwa kiwango cha asilimia 66 katika rika zote, na asilimia 71 miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.
Licha ya mafanikio, changamoto bado zipo
Mkurugenzi mkuu wa WHO Margaret Chan amesema mafanikio yaliyopatikana yametokana na juhudi kubwa katika usambazaji wa vifaa vya kinga na vya matibabu. Hata hivyo, mratibu wa mpango wa kupambana na Malaria duniani katika shirika hilo Pedro Alonso, amesema changamoto bado zipo licha ya mafanikio hayo.
''Pamoja na hatua hii ya kihistoria, bado yapo matatizo. La kwanza ni kwamba bado tuna idadi ya vifo zaidi ya laki nne, vitokanavyo na ugonjwa unaoweza kuzuiwa na unaotibika. La pili ni kwamba bado watu milioni 200 wanaambukizwa ugonjwa huo'', amesema mkurugenzi huyo.
Imeripotiwa kuwa zaidi ya nusu ya watu wote katika nchi zilizo Kusini ya Jangwa la Sahara wanalala ndani ya vyandarua vya kuzuia mbu.Kuongezeka haraka kwa uwezo wa kuchukua vipimo, na upatikanaji wa dawa za kutibu Malaria, ni miongoni mwa vigezo vingine vilivyochangia kupunguza Malaria.
Mbu wakaidi na Malaria sugu
Mkuu wa mpango wa kupambana na Malaria, Perdo Alonso, amesema changamoto nyingine kubwa inatokana na kuongezeka kwa mbu ambao hawaangamizwi na dawa ya kuuwa wadudu, hali ambayo amesema inatishia mapambano dhidi ya Malaria katika nchi nyingi. ''Malaria sugu isiyotibika kwa dawa inaweza kukwamisha juhudi za kuitokomeza Malaria'', amesema mkurugenzi huyo.
Asilimia zaidi ya 35 ya vifo vyote votokanavyo na Malaria ulimwenguni vinapatikana katika nchi mbili za kiafrika, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/APE
Mhariri: Mohammed Khelef