1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Watu 8 wamefariki kwa Marburg Tanzania

15 Januari 2025

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema mripuko wa ugonjwa unaoshukiwa kuwa ni Marburg umewauwa watu wanane katika eneo la vijijini kaskazini-magharibi mwa Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO- Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus azungumzia Virusi vya Marburg.Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Kupitia taarifa, Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema wanafahamu kwamba kufikia sasa kuna visa tisa vya watu walioambukizwa ikiwa ni pamoja na wanane waliokufa, na wanatarajia visa vya maambukizi kuongezeka katika siku kadhaa zijazo wakati ufuatiliaji wa ugonjwa huo unaendelea.

Hata hivyo, WHO imesema chimbuko la uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa huo kwenye mkoa wa Kagera, ulioko kaskazini-magharibi mwa Tanzania bado halijatambuliwa. Lakini tangazo hilo linajiri chini ya mwezi mmoja baada ya WHO kutangaza mlipuko wa miezi mitatu wa Marburg katika nchi jirani ya Rwanda.

Kama Ebola, virusi vya Marburg husababishwa na popo na husambaa kwa binaadamu kwa kugusana kwa karibu na maji maji ya mwili wa watu walioambukizwa au eneo lililoguswa na virusi hivyo, kama vile kitanda au mashuka yaliyotumiwa na mtu mwenye maambukizi.

Soma pia: Tanzania yatangaza kudhibitiwa kwa homa hatari ya Marburg

Bila ya kupata matibabu, Marburg inaweza kuwa na athari mbaya kwa hadi asilimia 88 miongoni mwa wanaougua ugonjwa huo. Dalili zake ni pamoja na homa, maumivu ya misuli, kuharisha, kutapika na wakati mwingine kifo kutokana na upotezaji mkubwa wa damu.

Hakuna chanjo iliyoidhinishwa au matibabu ya Marburg.

WHO imesema tathmini yake kuhusu hatari ya ugonjwa unaoshukiwa kuwa Marburg Tanzania uko katika ngazi ya kitaifa na kikanda, lakini bado haujafikia  kiwango cha juu Kimataifa. Mamlaka zinazohusika na masuala ya afya nchini Tanzania bado hazijatowa tamko lolote kuhusu ugonjwa huo.

WHO yahimiza tahadhari

Daktari akiwa ameshikilia bomba la kipimo cha damu cha virusi vya- Marburg.Picha: DmitriySk/Depositphotos/IMAGO

Mlipuko wa Marburg nchini Rwanda, uliripotiwa kwa mara ya kwanza Septemba 27, 2024 na kutangazwa kumalizika rasmi Desemba 20. Maafisa wa Rwanda waliripoti jumla ya vifo 15 na visa 66, na wengi wa walioathirika ni wafanyakazi wa huduma za afya ambao waliwahudumia wagonjwa wa kwanza.

Soma pia: Rwanda yatangaza kumalizika kwa mripuko wa kirusi cha Marburg

Mkoa wa Kagera ambao unanapakana na Rwanda, ulikumbwa na mlipuko wa kwanza wa ugonjwa wa Marburg mnamo Machi 2023, uliodumu kwa karibu miezi miwili, na kusababisha visa tisa na kuwauwa takriban watu watano.

Shirika la WHO pia linakadiria hatari ya kikanda kuwa "ya juu", kutokana na "eneo la kimkakati la Kagera ambalo ni kama kitovu cha usafiri chenye watu wengi wanaovuka mpaka kwenda Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo".

Kupitia mtandao wa X, mkuu wa WHO, amependekeza nchi jirani ziwe macho na zijitayarishe kudhibiti kesi zinazowezekana. Akisistiza kwamba hajapendekeza vikwazo vya kusafiri au kibiashara na Tanzania kwa wakati huu.

 

//dpa,AP, Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW