1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameomba radhi kwa waathiriwa.

22 Oktoba 2021

WHO imeahidi kuwa itafanya "mabadiliko makubwa" baada ya kashfa za unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji uliofanywa na wafanyakazi wa shirika hilo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kuwait | WHO Generaldirektor Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: Jaber Abdulkhaleg /AA/picture alliance

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya duniani WHO ameahidi Alhamisi hii kuwa atafanya "mabadiliko makubwa" katika shirika hilo baada ya kashfa za unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji uliofanywa na wafanyakazi wa shirika hilo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mnamo Septemba 28, tume huru ya uchunguzi ilitoa ripoti mbaya kwa WHO, ambayo iligundua kuwa wafanyakazi wake 21 kati ya 83 waliotuhumiwa, walitenda  kweli unyanyasaji huo dhidi ya watu kadhaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wa janga la Ebola mnamo kipindi cha mwaka 2018-2020, katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Tangu wakati huo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameomba radhi kwa waathiriwa.

Shirika hilo lenye nguvu la Umoja wa Mataifa, baada ya kuwekewa shinikizo na nchi wafadhili, limeahidi kutekeleza haraka mpango wake wa kukabiliana na vitendo hivyo. Mpango huo uliozinduliwa rasmi Oktoba 15 na kuwekwa hadharani mnamo siku ya Alhamisi unaahidi " kutostahmili kabisa unyanyasaji wa kingono na kutovumilia kamwe ukosefu wa kuchukua hatua."

Unyanyasaji wa kijinsia hauna nafasi

Katika taarifa yake, Dk Tedros amesema "amedhamiria kuhakikisha kwamba mateso ya manusura na familia zao yanatumika kama kichocheo cha mabadiliko makubwa katika mwenendo wa WHO", ambako zaidi ya watu 8,000 wanafanya kazi ulimwenguni kote. WHO inakusudia "kuunda utamaduni ambao ukandamizaji na unyanyasaji wa kijinsia hautokua na nafasi.

WHO imetenga kiasi cha awali cha dola milioni 7.6 ili kuimarisha uwezo wake wa kuzuia, kubaini na kujibu tuhuma za unyanyasaji wa kingono katika nchi kumi ikiwemo Afghanistan, Ethiopia na Venezuela. Mpango huo unadhihirisha hatua za haraka na msaada kwa waathirika na pia kuanza kwa kaguzi mfululizo. Katika miaka ya hivi karibuni, WHO inalenga "kubadilisha" uhalisia wa "mageuzi na miundo ya "utamaduni" wake.

"Matokeo ya kutisha"

WHO inakusudia pia kuchunguza mambo ya kitamaduni na kimuundo yaliyosababisha unyanyasaji wa kingono nchini DRC. Ripoti hiyo inadai kwamba "ukosefu wa usawa" ndani ya uongozi tendaji wa WHO, unaweza kuwa ulichangia kwa kiasi kikubwa matendo hayo ya unyanyasaji wa kijinsia.

Matokeo ya tume "ni ya kutisha", amesema Dk Tedros katika utangulizi wa ripoti hiyo na kusisitiza kuwa Unyanyasaji wa kijinsia "siku zote haukubaliki lakini huwa ni mbaya sana pale unapofanywa dhidi ya watu walio katika mazingira magumu na wahusika wakiwa ni wale wenye dhamana ya kuwalinda".

(AFP)