WHO yaazimia kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu ifikapo 2030
4 Oktoba 2017Hayo yamesemwa na mkurugenzi anayehusika na masuala ya dharura katika shirika hilo Dr. Peter Salama alipokuwa akizungumza na waandishi habari mjini Geneva.
Mkurugenzi huyo amesema shirika hilo lingeweza kuchukua hatua za haraka na kutuma chanjo zaidi ili kupambana na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa kipundupindu nchini Yemen mwaka huu.
Dr. Peter Salama bado ameeleza matumaini yake kwamba , "tunakaribia kufikia lengo," kuhusiana na ugonjwa huo unaoweza kuzuilika, unaosababishwa na vijidudu vilivyomo katika maji ambao umefikia maambukizi ya watu 700,000 na kusababisha zaidi ya vifo vya watu 2,000 mwaka huu.
Lengo ni moja kati ya malengo makubwa ya shirika la WHO kuutokomeza kabisa ugonjwa huo ama kupunguza kwa kiasi kikubwa ugonjwa huo. Juhudi kama hizo tayari zipo kwa ugonjwa wa kupooza, malaria, surua, na ukimwi. Hivi sasa, ni ugonjwa wa tetekuwanga tu ambao umekwisha tokomezwa katika uso wa dunia.
India na nchi zilizoko katika bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara zinakabiliwa na changamoto ya muda mrefu kupambana na kipindupindu.
Maeneo yanayozuka ugonjwa huo mara kwa mara
Maeneo kama Yemen inayokabiliwa na vita, ama Bangladesh, ambayo imewapokea zaidi ya wakimbizi 500,000 Waislamu wa Rohingya kutoka Mnyanmar, inakabiliwa na hali ambayo haitabiriki kwa urahisi. Mpango huo wa dunia unalenga katika kupambana na maeneo yanayozuka ugonjwa huo kila mara , ambako kila mwaka katika wakati ule ule , ugonjwa huo unazuka. Mpango huo unalenga kuboresha usafi wa maji na huduma za usafi , kwa kutumia chanjo za kunywa.
Mkakati huo unaweza kusaidia kutokometa kipindupindu katika mataifa 20 yaliyoathirika ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa WHO. India imeathirika kwa kiasi kikubwa ikiwa na zaidi ya kesi za maambukizi 675,000 kila mwaka, kwa mujibu wa shirika la WaterAid.
Pia ina idadi kubwa ya watu wanaoishi bila ya kuwa na uwezo wa kupata maji safi, na salama , na wengi wanaishi bila kuwa na vyoo sahihi.
Ethiopia na Nigeria , ambazo zinafuatia katika nafasi ya pili na tatu , pia zina idadi ya juu ya pili na ya tatu ya watu wanaoishi bila maji safi.
Mataifa mengine katika nchi kumi za juu ni pamoja na Haiti, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Tanzania , Kenya , Bangladesh, Uganda na Msumbiji.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga