1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yafungua kituo kipya cha kufwatilia magonjwa ya milipuko

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
1 Septemba 2021

Ujerumani na Shirika la Afya Ulimwenguni, zimezindua kituo kipya cha kimataifa cha shirika la WHO. Kituo hicho kilichopo mjini Berlin kitakuwa kinafuatilia tahadhari za mwanzo za magonjwa ya milipuko.

Berlin Kanzlerin Merkel und Ghebreyesus WHO
Picha: Michael Sohn/AP/picture alliance

Kituo hicho kipya kitawajumuisha wadau mbalimbali ulimwenguni kote, katika kuunda zana na kuhifadhi data zinazohitajika kuhusiana na maswala ya kujiandaa, kugundua na kukabiliana na hatari za magonjwa ambayo hutokea katika katika sehemu moja au hata yale yanayolipuka na kusababisha majanga katika maeneo mengi kwa wakati mmoja.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Jaber Abdulkhaleg /AA/picture alliance

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alitia saini hati ya makubaliano na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Charite, Heyo Kroemer. Hospitali hiyo iliyopo mjini Berlin inashirikiana pamoja na vitivo vya matibabu vya Chuo kikuu cha Humboldt na Chuo Kikuu Huria cha mjini Berlin. Wakati hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema.

Janga la COVID-19 limetuonyesha kuwa kuaminiana, ushirikiano na mshikamano ni vitu muhimu katika kukabiliana na vitisho vya pamoja kuhusiana na afya ya umma. Mkurugenzi huyo wa WHO aliongeza kuwa muhimu zaidi sasa kuliko hapo awali  ni fanya kazi na nchi nyingine na katika taaluma zote ili kujiandaa, kuzuia, kugundua na kuyashughulikia magojwa yanayojulikana pamoja na milipuko ya magonjwa ambayo yanaweza kusababisha majanga. 

Kutokana na athari zilizosababishwa na mlipuko wa virusi vya corona, wataalamu wa afya wanaamini kuwa janga jipya linaweza kuzuka wakati wowote hivyo basi wamesema mfumo mpya unapasa kuwepo utakaowezesha kutoa ishara za mapema ili uwekwe utaratibu madhubuti wa kufuatilia ishara hizo kwa ajili ya kuyadhibiti magonjwa ya milipuko kabla hayajaleta madhara.

Mnamo mwezi Mei wakati uamuzi huo ulipochukuliwa wa kuanzisha kituo hicho, kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema kuwepo kwa data ni kigezo cha msingi ili kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika siku za usoni. Kansela Merkel amesema kuwepo takwimu sahihi ambazo zimefanyiwa uchunguzi wa kina kwa kutumia zana, zenye uwezo au teknolojia ya akili bandia zitawezesha kupatikana ufahamu ambao peke yetu hatuwezi kuupata kwa haraka.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Picha: Michele Tantussi/REUTERS

Kituo hicho kipya cha kimataifa cha WHO kitatumia teknolojia ya akili bandia (AI) katika kuchambua idadi kubwa ya data, ikiwemo afya ya wanyama, magonjwa ya wanadamu yasiyo ya kawaida, mabadiliko katika tabia za binadamu, athari za  mabadiliko ya tabia nchi na pia mabadiliko katika idadi ya watu.

Taasisi za Ujerumani, pamoja na taasisi ya kudhibiti magonjwa ya Ujerumani, ya Robert Koch, na Hospitali ya Charite ya mjini Berlin, zitashirikiana kwa karibu katika mradi huo, pamoja na Taasisi ya Hasso Plattner ya Uhandisi wa kidijitali. Ujerumani itawekeza euro milioni 30 kwa ajili ya ufadhili wa kituo hicho kipya.

Chanzo:/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW