1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yahimiza dunia kushughulikia afya ya akili

20 Juni 2022

Shirika la Afya Duniani, WHO limetoa wito wa mabadiliko makubwa kufanyika katika mifumo ya afya ya akili duniani, likisema kuna ongezeko kubwa la watu walio na matatizo ya akili duniani tangu kuanza kwa janga la COVID-19

Mailand Gucci Fashion Show Mental Health
Picha: Getty Images for Gucci

Shirika hilo la WHO limesema matatizo ya msongo wa mawazo na sonona yameongezeka kwa asilimia 25 katika mwaka wa kwanza wa janga la corona.

Katika ripoti yake kuhusu matatizo ya akili duniani ambayo ni kubwa kabisa kufanywa na shirika hilo tangu kuanza kwa karne ya 21, imesema takriban watu bilioni moja au mtu mmoja kwa kila watu wanane duniani wamekuwa wakiishi na matatizo ya akili tangu mwaka 2019 kabla ya janga la corona kuanza.

Ripoti hiyo imeonya kuwa watu walio na matatizo sugu ya afya ya akili wanakufa miaka 10 au 20 mapema kuliko watu wengine.

Moja ya sababu kubwa zinazosababisha msongo wa mawazo ni kunyanyaswa kingono ukiwa na umri mdogo na hata uonevu unaofanywa katika umri huo. Sasa shirika hilo limetaka hatua za haraka kuchukuliwa kushughulikia masuala haya yote mawili kupitia taasisi za kijamii, kusaidia familia zisizojiweza na kubuni mipango itakayowasaidia wenye uhitaji mashuleni.

Jinsi ya kumtambua mgonjwa wa afya ya akili

03:13

This browser does not support the video element.

Ukosefu wa usawa kijamii na kiuchumi, vita, mgogoro wa mabadiliko ya tabia nchi, na vitisho vya afya kama majanga yote haya yameorodheshwa kama mambo yanayochangia mtu kupata matatizo ya akili.

Mark Van Ommeren, mkuu wa kitengo cha afya ya akili katika shirika la WHO amesema ni muhimu kuhakikisha jamii inakomesha unyanyasaji majumbani na hata kujitolea kuimarisha afya ya akili mashuleni na hata kwenye maeneo ya kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema maisha ya kila mtu yanamgusa mtu mwenye matatizo ya akili.

Amesema mtu akiwa na afya njema ya akili inamaanisha afya njema kimwili na ndio maana ripoti hii mpya inatoa wito wa kufanyika mabadiliko makubwa duniani kwa nia ya kupunguza watu wanaokabiliwa na matatizo ya aina hiyo.

Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema uwekezaji katika afya ya akili ni uwekezaji katika maisha bora na siku zijazo kwa wote.

Mwandishi: Amina Abubakar

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW