1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yahimiza tahadhari juu ya Ebola, Guinea na DRC

16 Februari 2021

Mamlaka nchini Guinea na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zinafanya juu chini kudhibiti miripuko miwili tofauti ya ugonjwa wa ebola. 

Demokratische Republik Kongo | Ebola Ausbruch | Krankenhaus
Picha: Al-hadji Kudra Maliro/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa shirika hilo la Afya Duniani-WHO Margaret Harris, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva leo kwamba, chanjo na vifaa vya matibabu vinasafirishwa kupelekwa katika nchi hizo mbili Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kupiga jeki juhudi za kudhibiti miripuko hiyo.

Mkuu wa shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema shirika lake linafany akazi kwa ushirikiano na mataifa hayo mawili kukabili miripuko hiyo.

"Ninafurahi kusema kwamba chanjo imeanza kutolewa DRC. Hadi sasa watu 43 wameshachanjwa miongoni mwa jumla ya 149 waliotangamana na waathirika, wakiwemo pia 20 waliopokea chanjo wakati wa mripuko wa uliopita wa 2019." Amesema Ghebreyesus.

Guinea, nchi ya magharibi mwa Afrika imesharekodi maambukizi ya watu kumi pamoja na vifo vya watu watano tangu mripuko wa sasa kuanza kusini mashariki mwa taifa hilo. Maafisa wa afya nchini humo wamesema hayo leo.

Mhudumu wa afya akimpima mtu viwango vya joto mwilini katika hospitali ya Matanda mjini Butembo ambako kisa cha kwanza cha ebola kiligunduliwa Februari 11, 2021.Picha: Al-hadji Kudra Maliro/AP Photo/picture alliance

Soma pia: Congo na vita visivyokwisha dhidi ya Ebola

Mamia ya waliokaribiana na wagonjwa wafuatiliwa

Wizara ya Afya ya Guinea imesema imeshawatambua watu 115 waliokaribiana na wagonjwa ambao wamethibitishwa katika mji wa Nzerekore, na wengine 10 katika mji mkuu Conakry tangu Jumapili.

Kulingana na WHO, katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, watu wanne wamegunduliwa kuambukizwa ebola, na wengine wawili wamefariki.

Ugonjwa huo wa virusi hatari husababisha joto mwilini na mara nyingi husababisha watu kuvuja damu kwa wingi ndani ya mwili na kifo.

Msemaji wa WHO Margaret Harris ameongeza kwamba maafisa wa afya nchini Guinea na DRC wana tajriba ya kushughulikia ebola kutokana na miripuko iliyopita.

Afisa wa afya akagua eneo la karantini katika hospitali ya Matanda Butembo ambako kisa cha kwanza cha ebola kiligunduliwa Februari 11, 2021.Picha: Al-hadji Kudra Maliro/AP Photo/picture alliance

WHO yazitaka nchi sita ikiwa ni pamoja na Sierra Leone, na Liberia kuchukua tahadhari.

Nchi jirani kama Cote di'Voire, Mali na Sierra Leone hapo jana zilianzisha mipango ya kuzuia uwezekano wa kuenea kwa virusi hivyo kwa kuimarisha sheria za mipakani.

Kulingana na Margaret Harris, tathmini ya jeni za sampuli ya virusi vya ebola kutoka Congo na Guinea inaendelea kufanywa ilikubaini aina ya virusihivyo na vilianzia wapi.

Wakati wa mripuko uliopita wa ebola Magharibi mwa Afrika, zaidi ya watu 28,000 walifariki. Vifo 11,310 viliripotiwa Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Mripuko wa mwaka jana wa ugonjwa wa ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ulisababisha vifo vya watu 2,229 lakini watu 1,162 walipona.

(DPAE, AFPE, RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW