WHO yaidhinisha chanjo ya kwanza dhidi ya Malaria
7 Oktoba 2021Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameitaja hatua hiyo kuwa ya "kihistoria" baada ya mkutano ambao wataalamu wa makundi mawili ya ushauri wa shirika hilo walitoa mapendekezo yao.
"Malaria imekuwa nasi kwa milenia na ndoto ya chanjo ya malaria imekuwa ya muda mrefu lakini isiyoweza kufikiwa. Leo, chanjo ya malaria ya RTS, S, ikitengenezwa kwa zaidi ya miaka 30, inabadilisha historia ya afya ya umma . Chanjo hii ni zawadi kwa ulimwengu, lakini thamani yake itaonekana zaidi barani Afrika kwa sababu huko ndiko kuna mzigo zaidi mkubwa wa malaria".
WHO imesema uamuzi wake umetokana na matokeo ya utafiti unaoendelea katika nchi za Ghana, Kenya na Malawi ambao uliwafuatilia watoto zaidi ya 800,000 waliopatiwa chanjo ya Malaria tangu mwaka 2019. Kiasi cha dozi milioni 2.3 za chanjo hiyo zilitolewa kwa watoto wadogo katika nchi hizo tatu. Programu hiyo ilifuatiwa na majaribio kadhaa ya kliniki katika nchi saba za Afrika. Chanjo hiyo inayojulikana kwa jina la Mosquirix, imetengenezwa na kampuni ya madawa ya Uingereza GlaxoSmithKline (GSK) mwaka 1987.
Wakati ikiwa ndio chanjo ya kwanza kuidhinishwa dhidi ya ugonjwa huo, bado inakabiliwa na changamoto. Chanjo hiyo ina ufanisi wa asilimia 30 na inahitaji hadi dozi nne wakati ulinzi wake ukififia baada ya miezi kadhaa. Hata hivyo wanasayansi wanasema inaweza kuleta matokeo makubwa dhidi ya ugonjwa wa Malaria barani Afrika, ambako maambukizi yanatajwa kufikia zaidi ya milioni 200 na vifo 400,000 kwa mwaka.
Malaria ni ugonjwa unaotajwa kuwa mbaya zaidi kuliko COVID-19 barani Afrika. Kulingana na takwimu za WHO, ugonjwa huo uliua waafrika wapatao 386,000 mnamo 2019, ikilinganishwa na vifo 212,000 vya COVID-19 katika kipindi cha miezi 18.
Shirika hilo la afya ulimwenguni linasema asilimia 94 ya visa na vifo vya malaria vinatokea Afrika, bara lenye watu bilioni 1.3. Ugonjwa huo husababishwa na vimelea vinavyoambukizwa kwa watu kutokana na kuumwa na mbu. Dalili zake ni pamoja na homa, kutapika na uchovu.
Wataalamu wanasema changamoto kubwa sasa itakuwa ni uhamasishaji wa kukusanya fedha kwa ajili ya uzalishaji na ugavi wa chanjo katika nchi maskini zaidi duniani. Kampuni inayotengeneza chanjo hizo hadi kufikia sasa imeahidi kuzalisha dozi milioni 15 kwa mwaka kufikia mwaka 2028. Utafiti wa soko la dunia ukiongozwa na WHO mwaka huu ulikadiria mahitaji ya chanjo za Malaria yatakuwa kati ya dozi milioni 50 hadi 110 kwa mwaka kufikia 2030.