1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaidhinisha kipimo cha kwanza cha mpox

4 Oktoba 2024

Shirika la Afya Ulimwenguni limeidhinisha kipimo ambacho kitatumiwa kupima ugonjwa wa Mpox kwenye maabara. Hicho ni kibali cha kwanza kutolewa na WHO

Shirika la Afya Duniani WHO
Nembo ya Shirika la Afya Duniani WHOPicha: Denis Balibouse/REUTERS

Kampuni ya Abbott Molecular yenye makao yake makuu Illinois, kaskazini mwa jiji la Chicago nchini Marekani ndiyo imepewa kibali na WHO kusambaza vifaa vya upimaji ambavyo vinatoa majibu katika muda mfupi (PCR).

Shirika la afya duniani limesema kipimo hicho kinachoitwa Alinity m MPXV,  kina uwezo wa kutambua vinasaba yaani DNA ya virusi vya mpox kutoka kwenye majimaji ya ngozi ya binadamu mara inapopanguswa na kijipamba maalum.

Soma Zaidi: Ghana yathibitisha maambukizo ya kwanza ya mpox

Shirika la Afya Duniani WHO limeongeza kusema kwamba kipimo hicho cha kwanza cha ugonjwa wa mpox, kitayasaidia mataifa duniani yanayopambana kudhibiti maradhi hayo hatari.

Mtoto aliyeambukizwa mpox anapata matibabu katika hospitali ya kwenye eneo la NyiragongoPicha: Zanem Nety Zaidi/Xinhua/IMAGO

Zaidi ya watu 800 wamekufa barani Afrika kutokana na ugonjwa wa mpox na tayari mataifa 16 yamethibitisha kugunduliwa watu walioambukizwa maradhi hayo.

Katika bara la Afrika nchi iliyoathiriwa zaidi ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika hospitali ya Lwiro iliyo kwenye eneo la Kivu Kusini ndiyo kama kitovu cha mlipuko huo wa ugonjwa wa mpox. Kuna msongamano mkubwa wa wagonjwa kiasi kwamba kina mama wanalazimika kulala wawili au zaidi kwenye kitanda kimoja.

Soma Zaidi: Makahaba, wachimba madini wachochea kusambaa kwa mpox Kongo

Ingawa madaktari katika eneo hilo wameshawahi kushughulikia virusi vya mpox hapo awali, lakini wanasema mlipuko wa mara hii ni tofauti. Daktari Imani Banyanga amesema kwa sasa watoto ndio wengi ambao ni wagonjwa. Amesema watoto hao wengi wao ni wale walio chini ya miaka mitano na wengine wachanga wenye umri wa wiki mbili au wiki tatu tayari wanaugua mpox.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa WHO, Yukiko Nakatani, amesema kuongeza upatikanaji wa bidhaa bora za matibabu ni msingi wa juhudi za shirika la afya duniani katika kuzisaidia nchi kudhibiti kuenea kwa virusi na kuwalinda watu wao, haswa katika maeneo ambayo hayana huduma nzuri za afya.

Soma Zaidi: Africa CDC: Zaidi ya dola milioni 800 zimeahidiwa kwa Afrika kukabiliana na Mpox

Ugonjwa wa Mpox ambao awali ulijukana kama ugonjwa wa homa ya nyani, husababishwa na virusi vinavyoambukizwa kwa wanadamu kutoka kwa wanyama walioambukizwa lakini pia binadamu kwa binadamu wanaweza kuambukizana kwa kukaribiana kimwili.

Ugonjwa huo husababisha homa, kuumwa na misuli na mapele kwenye ngozi yaliyo kama majipu, na unaweza kusababisha kifo.

Chanzo: AFP